KLABU ya Juventus ya Italia imefanikiwa kupiga hatua moja muhimu kuelekea nusu fainali ya michuano ya Europa League baada ya kufanikiwa kushinda bao 1-0 dhidi ya Lyon katika mchezo wa mkondo wa kwanza ya robo fainali. Katika mchezo huo bao pekee lilifungwa na Leonardo Bonucci katika dakika ya 85 hivyo kufanya vinara hao wa Ligi Kuu nchini Italia kuendelea kupewa nafasi ya kutinga fainali ya michuano hiyo itakayochezwa Mei 14. Katika mechi za michuano hiyo zilizochezwa jana FC Basel ya Switzerland nao walifanikiwa kujiweka katika nafasi nzuri baada ya kuitandika Valencia mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa katika uwanja mtupu. Timu za Ureno Benfica na Porto nazo zimejitengenezea mazingira mazuri ya kusonga mbele baada ya kushinda mechi zao za mkondo wa kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya AZ Alkmaar na Sevilla.
Friday, April 4, 2014
Wednesday, April 2, 2014
KABOUL AKANUSHA TTESI ZA KUJIUNGA NA ARSENAL.
BEKI mahiri wa klabu ya Tottenham Hotspurs, Younes Kaboul amesisitiza kuwa tetesi za yeye kuhamia Arsenal sio za ukweli kwa asilimia 100. Mapema leo gazeti la Daily Star la Uingereza liliripoti kuwa Kaboul amewaambia marafiki zake anataka kujiunga na Arsenal wakati mkataba wake utakapomalizika mwishoni mwa msimu huu. Lakini beki huyo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa hana mpango huo kama ilivyoelezwa na gazeti hilo. Kaboul anaonekana kujitetea yasije kumkuta yaliyomkuta Sol Campbell mwaka 2001 ambaye alikataa kusaini mkataba mpya na Spurs na badala yake kuichagua Arsenal hatua ambayo ilipelekea kuchukukiwa na mashabiki wa klabu hiyo.
WACHEZAJI NGORONGORO HEROES WAAHIDI USHINDI.
NAHODHA wa timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes), Aishi Manula amesema wamejipanga kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mechi dhidi ya Kenya itakayochezwa Jumapili (Aprili 6 mwaka huu) katika mji wa Machakos. Akizungumza leo (Aprili 2 mwaka huu) kwenye hafla ya kukabidhiwa bendera kwa timu hiyo kwenye ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Manula ambaye pia anaidakia timu ya Azam alisema lengo lao ni kufanya vizuri kwenye mechi hiyo. Naye Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Michezo, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yasoda akikabidhi bendera hiyo, aliwataka wachezaji hao kujituma na kutanguliza uzalendo mbele bila kusahau kuwa mchezo wa mpira wa miguu ni ushirikiano. Alisema Tanzania ina wachezaji wengi wenye vipaji, hivyo waliopata fursa ya kuwemo Ngorongoro Heroes wakati huu wajue kuwa wamepata bahati, na wanatakiwa kufahamu kuwa wao ni wawakilishi wa Tanzania, na Watanzania wana kiu ya kusikia matokeo ya mechi hiyo. Ngorongoro Heroes inayofundishwa na John Simkoko inaondoka kesho (Aprili 3 mwaka huu) saa 4.30 asubuhi kwa ndege ya Kenya Airways, na mara baada ya kuwasili itakwenda moja kwa moja kwenye hoteli ya Garden iliyopo Machakos ambayo ndiyo imepangiwa kufikia na Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF). Wachezaji waliopo kwenye msafara huo unaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF), Ayoub Nyenzi ni Abrahman Mohamed, Aishi Manula, Ally Idd, Ally Mwale, Athanas Mdamu, Ayoub Semtawa, Bryson Raphael na Edward Manyama. Wengine ni Gadiel Michael, Hamad Juma, Hassan Mbande, Ibrahim Ahmada, Idd Ally, Kelvin Friday, Michael Mpesa, Mohamed Ibrahim, Mudhathir Yahya, Pato Ngonyani, Peter Manyika na Salum Mineli.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI YACHACHAFYA BRAZIL.
TIMU ya Watoto wa Mitaani ya Tanzania kutoka Kituo cha Mwanza inaendelea vizuri katika mashindano ya Kombe la Dunia kwa Watoto wa Mitaani yanayoendelea Rio de Janeiro nchini Brazil ambapo katika mchezo wake wa kwanza ilitoka sare ya mabao 2-2 na Burundi. Juzi (Machi 31 mwaka huu), timu hiyo inayoongozwa na mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutoka Mkoa wa Mwanza, John Kadutu ilicheza mechi mbili. Katika mechi ya kwanza iliifunga Argentina mabao 3-0 na baadaye ikailaza Nicaragua mabao 2-0. Michuano hiyo ya siku kumi inashirikisha timu kumi. Mbali ya Tanzania, nyingine ni Argentina, Burundi, India, Kenya, Liberia, Marekani, Mauritius, Misri na Pakistan. Kwa wasichana ni Afrika Kusini, Brazil, El Salvador, Indonesia, Msumbiji, Nicaragua, Philippines, Uingereza na Zimbabwe.
SPURS KUHAMIA UWANJA MPYA 2017.
KLABU ya Tottenham Hotspurs inategemea kuhamia katika uwanja wake mpya wenye uwezo wa kubeba mashabiki 58,000 ifikapo mwaka 2017. Uwanja huo mpya unatarajiwa kuwa pembeni ya uwanja wao wa sasa wa White Hart Lane ambao unauwezo kuingiza mashabiki 36,000. Klabu hiyo inategemea kutoa zabuni kwa ajili ya ujenzi wake baada mwaka huu huku wakitegemea ufunguzi kuwa katikati ya mwaka 2017. Habari za uwanja mpya zimekuja ikiwa ni siku baada ya Tottenham kutangaza faida ya paundi milioni 1.5 katika mwaka wao wa fedha uliopita.
BARCELONA YAFUNGIWA KUSAJILI NA FIFA.
KLABU ya Barcelona imefungiwa kusajili wachezaji kwa vipindi viwili vya usajili na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA kwa kukiuka taratibu za kimataifa zinazohusu usajili wa wachezaji chini ya umri wa miaka 18. Hatua hiyo imekuja kufuatia uchunguzi wa awali uliofanywa na shirikisho hilo kupitia mfumo wake wa uhamisho-TMS kwa mwaka uliopita. Barcelona wamekutwa wamekiuka vifungu kadhaa kuhusiana na uhamisho wa kimataifa sambamba na usajili wa wachezaji walio chini ya umri ambao sio raia wa Hispania. Uchunguzi huo ulihusisha wachezaji kadhaa walio chini ya umri huo ambao waliandikishwa na kushiriki mashindano wakiwa na timu hiyo katika kipindi cha mwaka 2009-2013.
MWAMUZI ALIYEFANYA MADUDU MECHI YA ARSENAL NA CHELSEA APEWA KUCHEZESHA NUSU FAINALI KOMBE LA FA.
MWAMUZI Andre Marriner ameteuliwa kuchezesha mechi ya nusu fainali ya Kombe la FA kati ya Hull City na Sheffield United itakayofanyika katika Uwanja wa Wembley Aprili 13 mwaka huu. Marriner mwenye umri wa miaka 43 alihusika katika tukio la kutoa kadi nyekundu kwa mchezaji tofauti kwenye mchezo kati ya Chelsea na Arsenal uliochezwa mwezi uliopita. Mwamuzi huyo alimtoa Kieran Gibbs wa Arsenal badala ya Alex Oxlade-Chamberlain ambaye ndiye aliyeshika mpira uliopigwa na Eden Hazard katika mchezo huo lakini kadi hiyo ilifutwa baada kukata rufani. Hata hivyo Marriner aliomba radhi kwa mkanganyiko huo uliotokea kwenye mchezo huo ambao Arsenal waliogeshwa mabao 6-0 na Chelsea. Kwa upande wa nusu fainali fainali nyingine ya michuano hiyo ambayo itazikutanisha timu za Arsenal na Wigan Athletic mwamuzi atakuwa ni Michael Oliver.
Subscribe to:
Posts (Atom)






