Friday, January 2, 2015

TETESI ZA USAJILI: MAN UNITED WAMTENGEA FUNGU POGBA, MADRID NAO WAINGIA MBIO ZA KUMUWANIA BONY.

KATIKA kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo la usajili taarifa mbalimbali zimekuwa zikivuma huku kule kuhusiana na mchezaji huyu na yule. Mojawapo ya habari zilizopamba vichwa vya habari vya baadhi ya magazeti hivi leo ni pamoja na taarifa kuwa klabu ya Manchester United imepanga kuvunja kibubu na kumrejesha kiungo Paul Pogba kutoka klabu ya Juventus. Kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa aliondoka United kuelekea Juventus mwaka 2012 lakini sasa anaweza kurejea Old Trafford baada ya kuripotiwa kuwa meneja Louis van Gaal yuko tayari kutoa kitita cha euro milioni 90. Juventus nao wanafikiria mchezaji atakayechukua nafasi ya mshambuliaji wao Carlos Tevez wakati atakapoondoka. Tevez ameshaweka wazi kuwa hana mpango wa kuongeza mkataba katika timu hiyo pindi utakapomalizika na Juventus wanadhaniwa kuwa wanaweza kumuwinda Radamel Falcao ili kuziba nafasi hiyo. Klabu ya Real Madrid nayo imeingia katika mbio za kumuwinda mshambuliaji wa Swansea City Wilfried Bony. Madrid wanamtaka Bony ili aweze kusaidiana na Karim Benzema huku Manchester City, Liverpool na Tottenham Hotspurs nazo zikimuwinda kwa karibu nyota huyo wa kimataifa wa Ivory Coast. Kuna taarif nyingine kutoka nchini Uingereza kuwa mmiliki wa klabu ya Chelsea Roman Abromovich anatarajia kujaribu kumsajili Lionel Messi kama Barcelona haitashinda taji lolote msimu huu. Meneja wa Chelsea Jose Mourinho ametoa ombi la kusajiliwa kwa mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Argentina ambaye amewahi kushinda mataji manne ya Ballon d’Or.

ARSENAL KUISIKILIZA INTER KAMA WAKIONGEZA OFA YA KUMTAKA PODOLSKI.

KLABU ya Arsenal itafikiria ofa iliyoimarishwa kutoka Inter Milan kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa kimataifa wa Ujerumani Lukas Podolski. Podolski mwenye umri wa miaka 29 ameshindwa kupata namba katika kikosi cha kwanza cha Arsenal msimu huu huku akiukosa mchezo dhidi ya Southampton jana kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya nyonga. Meneja wa klabu hiyo Arsene Wenger amesema ofa ya kwanza waliyotoa Inter ilikuwa ndogo hivyo kama wakirudi tena na fungu la kueleweka wataangalia uwezekano wa kufanya biashara. Podolski alinunuliwa na Arsenal kwa kitita cha paundi milioni 11 akitokea klabu ya Cologne mwaka 2012 lakini amefanikiwa kuanza kucheza mechi 39 pekee katika akiwa chini ya Wenger. Mshambuliaji huyo amefunga jumla ya mabao 31 katika mechi 82 alizoichezea Arsenal katika mashindano yote.

SHABIKI ALIYEKWENDA KUMVAA WENGER ATIWA MBARONI.

SHABIKI mmoja amekamatwa baada ya kumvaa meneja wa Arsenal Arsene Wenger wakati wa mchezo wa Ligi Kuu mbao wlaifungwa na Southampton kwa mabao 2-0 jana. Shabiki huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa akienda kumvaa Wenger mwenye umri wa miaka 65 lakini alizuiwa na mabaunsa kabla ya polisi wa Hampshire hawajamata. Taarifa ya klabu ya Southampton imedai kuwa shabiki huyo alikuwa mshabiki wa Arsenal ambaye alikuwa amekaa jukwaa la mashhabiki wa nyumbani lakini Wenger anadhani alikuwa mshabiki wa Saints. Tukio hilo linakuja baada ya Wenger kushambuliwa na mashabiki wa Arsenal wakati akipanda treni baada ya kipigo dhidi ya Stoke Desemba mwaka jana. Akihojiwa baada ya tukio hilo Wenger amesema anadhani shabiki huyo hakuwa na nia ya kumdhuru kwani hakumsikia hata akisema lolote.

AFCON 2015: MALI KUMKOSA DIABATE.

MSHAMBULIAJI wa klabu ya Bordeaux ya Ufaransa, Cheick Diabate anatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa goti ambao utamfanya kushindwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa ya Mali kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika. Diabate ambaye ndio anaongoza akiwa ameufunga mabao nane katika klabu yake msimu huu, wiki iliyopita alitajwa katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 wa Mali kwa ajili ya michuano hiyo itakayofanyika huko Guinea ya Ikweta. Bordeaux ilitangaza jana kuwa nyota huyo mwenye umri wa miaka 26 alikubali kufanyiwa upasuaji huo baada ya kushauriwa na mtalaamu jijini Marseille mwezi uliopita. Taarifa hiyo itakuwa pigo kubwa kwa kocha wa Mali Henryk Kasperczak kwani alikuwa akimtegemea mshambuliaji huyo kwa ajili ya michuano hiyo ya mwaka huu. Mali ambao katika michuano iliyopita walimaliza katika nafasi ya tatu, wamepangwa katika kundi gumu la D wakiwa sambamba na timu za Ivory Coast, Cameroon na Guinea.

KAMA KAWAIDA YAKE MOURINHO ALIA NA WAAMUZI BAADA YA KICHAPO CHA 5-3 KUTOKA KWA SPURS.

MENEJA wa klabu ya Chelsea, Jose Mourinho anaamini kikosi chake kingeweza kuichapa Tottenham Hotspurs kama wangezawadiwa penati ambayo ingewafanya kuongoza katika mchezo huo. Baada ya Diego Costa kuifungiwa Chelsea bao la kuongoza, timu hiyo ilinyimwa penati na mwamuzi Phil Dowd wakati Jan Vertonghen aliposhika mpira katika eneo la hatari, na baadae kuja kupoteza mchezo huo kwa kufungwa mabao 5-3. Mourinho alimlaumu mwamuzi wa mchezo huo kwa kushindwa kutoa penati hiyo kwani ingewapa nafasi nzuri ya kushinda mchezo huo. Hata hivyo baadhi wachambuzi wa soka wameshindwa kukubaliana na Mourinho wakidai kuwa haikustahili kuwa penati hivyo mwamuzi alikuwa sahihi. Chelsea ambao walikuwa wakiongoza kwa tofauti ya alama nane katika msimamo wa Ligi Kuu Novemba mwaka jana sasa wako juu ya Manchester City kutokana na mpangilio wa herufi kufuatia kipigo hicho cha jana.

XAVI AIPONDA CAS KUFUATIA UAMUZI WAO.

KIUNGO mahiri wa Barcelona Xavi, ameiponda Mahakama ya Michezo ya Kimataifa-CAS kwa uamuzi wake wa kutupilia mbali rufani ya klabu hiyo wakipinga adhabu ya kufungiwa kusajili na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Barcelona walipewa adhabu hiyo kutokana na kupatikana na hatia ya kusajili wachezaji chini ya umri wa miaka 18 kutoka nje ya Hispania na baadae kukata rufani CAS ambayo katika maamuzi yake ilitupilia mbali. Uamuzi huo utaifanya Barcelona kushindwa kusajili mchezaji wa aina yeyote kwa mwaka huu na Xavi anadhani adhabu hiyo haijatenda haki. Xavi ambaye ni nahodha wa Barcelona amesema wote wameshangazwa na uamuzi huo wa CAS kwani walitegemea kupunguza adhabu hiyo ambayo inaonekana kuwa kali kuliko kosa lenyewe. Hata hivyo Xavi anaamini kuwa Barcelona bado ina vipaji vya kutosha vya kuifanya kuwa tishio katika kila mchezo wanaocheza.

GERRARD ATANGAZA KUONDOKA LIVERPOOL MWISHONI MWA MSIMU.

NAHODHA wa klabu ya Liverpool, Steven Gerrard ametaja uamuzi wake wa kuondoka katika timu hiyo mwishoni mwa msimu huu kama mgumu kuwahi kufanya katika maisha yake. Gerrard mwenye umri wa miaka 34 anatarajia kumaliza mkataba wake katika majira ya kiangazi baada ya kujiunga na klabu hiyo akiwa na miaka tisa na kufunga mabao 180 katika mechi 695 alizowahi kuichezea Liverpool. Akihojiwa na wanahabari Gerrard amesema uamuzi huo ni mgumu kuwahi kufanya katika yake na ambao yeye pamoja na familia yake wamekuwa wakiuandaa kwa kipindi kirefu. Kiungo huyo aliendelea kudai kuwa anaweza kuendelea kucheza lakini haitakuwa katika timu ambayo inayoweza kukutana na Liverpool katika mechi zake. Gerrard anahisishwa na kuhamia katika Ligi Kuu nchini Marekani-MLS mara baada msimu wao soka Uingereza utakapomalizika.