Tuesday, June 2, 2015

HATIMAYE BLATTER AAMUA KUACHIA NGAZI FIFA.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter ametangaza kujiuzulu wadhifa wake huo na kuitisha mkutano mkuu wa dharura ambao utafanyika uchaguzi wa kutafuta mbadala wake.Blatter mwenye umri wa miaka 79, alitangaza uamuzi wake huo mbele ya wana habari leo baada ya Katibu Mkuu wake Jerome Valcke mapema kuhusishwa na tuhuma za kuidhinisha dola milioni 10 kwenda kwa makamu wa zamani wa FIFA Jack Warner.Akitangaza uamuzi wake huo Blatter amesema amefikiria kwa makini kuhusu urais wake na miaka 40 ambao amekuwa ndani ya Shirikisho hilo na kwa mapenzi makubwa aliyonayo kwa mchezo wa soka ameamua kuachia ngazi.Blatter aliendelea kudai kuwa kingine kilichomsukuma kuachia ngazi ni kuona watu wengi hawadhani kama anaweza kulipeleka shirikisho hilo mbele jambo ambalo anaona lingerudisha nyuma mchezo wa soka kama angendelea kukaa madarakani.Uchaguzi kwa ajili ya kuziba nafasi ya Blatter unatarajiwa kupangwa kufanyika kati ya Desemba mwaka huu ay Machi mwakani.

POGBA ADAI KUWA NA NDOTO ZA KUCHEZA SAMBAMBA NA MESSI.

KIUNGO wa Juventus, Paul Pogba amekiri kuwa ana ndoto za kucheza sambamba na mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi.Nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa kwa kipindi kirefu amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka jijini Turin huku Barcelona na Real Madrid zikitajwa kuwa na nia ya kumsajili.Pogba sasa ameweka wazi jinsi anavyoihusudu Barcelona ambao watakuwa wapinzani wao katika mchezo wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya Jumamosi hii.Nyota huyo alikaririwa akidai kuwa kucheza pamoja na Messi itakuwa ni kutimiza ndoto zake kuwa kweli kwasababu ni mchezaji bora duniani.Pogba aliendelea kudai kuwa anajua Barcelona wanapewa nafasi kubwa kuwa mabingwa katika mchezo wao ujao lakini watafanya kila wawezalo kuhakikisha wanashinda katika mchezo huo.

NI NGUMU KUZIKATALIA BARCELONA AU REAL MADRID.

MSHAMBULIAJI nyota wa Lyon, Alexandre Lacazette amesisitiza kuwa hajapata uamuzi juu ya mustakabali wake lakini amekiri kuwa itamuwia vigumu kukataa kwenda katika timu kama Barcelona au Real Madrid.Lacazette mwenye umri wa miaka 24 ndio mfungaji anayeongoza katika Ligi Kuu ya Ufaransa msimu huu, aliwa ameifungia Lyon mabao 27 na kuifanya kumaliza katika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi.Kutoka na hilo nyota huyo wa kimataifa wa Ufaransa amekuwa akihusishwa na tetesi za kutakiwa na vilabu kadhaa lakini mwenyewe amesema anataka kupumzika na kumuachia wakala wake kuzungumza na timu zinazomuhitaji.Akihojiwa Lacazette amesema hajaamua lolote mpaka sasa kwani anaenda zake likizo na kumuachia wakala wake masuala yote.

LLORIS AJINADI KUONDOKA SPURS.

GOLIKIPA wa Tottenham Hotspurs Hugo Lloris amethibitisha kuwa hakuna kiwango chochote cha ada kilichowekwa kwake na klabu hiyo kufuatia taarifa kuwa Manchester United inahitaji kumsajili.Kulikuwa na taarifa kutoka Ufaransa zilizodai kuwa golikipa huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa amewekewa kiwango cha euro milioni 20 kwa timu itakayomuhitaji kama Spurs wakishindwa kufuzu michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.Lloris amebainisha kuwa anafanya mawasiliano ya karibu na mwenyekiti wa Spurs Daniel Levy na kusisitiza kuwa atapewa taarifa kama kuna ofa yeyote itakayotolewa kwake majira haya ya kiangazi.Akiulizwa kuhusiana na kiwango hicho kilichowekwa, Lloris amesema katika mkataba wake hakuna kipengele kama hicho.Golikipa huyo aliendelea kudai kuwa kama ikitoka ofa nzuri ambayo itaziridhisha pande zote mbili anadhani anaweza kuondoka lakini kwasasa bado ataendelea kuwepo hapo kwani amekuwa na mahusiano mazuri na viongozi.

SINA BIFU NA SUAREZ – CHIELLINI.

BEKI mahiri wa Juventus, Giorgio Chiellini amesema atashikana mikono na Luis Suarez wakati watakapokutana kwa mara ya kwanza toka nyota huyo wa Uruguay amng’ate katika michuano ya Kombe la Dunia mwaka jana.Mshambuliaji huyo wa Barcelona mwenye umri wa miaka 28 alifungiwa miezi minne kwa kosa hilo la kumng’ata Chiellini begani wakati wa mchezo wa makundi dhidi ya Italia Juni mwaka jana.Wawili hao wanatarajiwa kukutana katika mchezo wa fainali ambao utazikutanisha klabu zao Jumamosi hii jijini Berlin, Ujerumani.Akihojiwa Chiellini mwenye umri wa miaka 30 amesema hana tatizo lolote na Suarez na pindi watakapokutana atafurahia kushikana naye mikono na kumkumbatia.Mchezaji mwenzake na Chiellini katika klabu hiyo Patrice Evra alikataa kushikana mikono na Suarez baada ya kufanyiwa vitendo vya kibaguzi na nyota huyo wakati akiwa Liverpool nay eye akiwa Manchester United.

BADO SIJAJUA MUSTAKABALI WANGU MSIMU UJAO – BENTEKE.

MSHAMBULIAJI wa Aston Villa Christian Benteke amesema atamuachia wakala wake mustakabali wake kufuatia tetesi za kutakiwa na klabu za Liverpool na Chelsea.Benteke mwenye umri wa miaka 24, alikuwa amewavutia wengi msimu huu kutoka na kiwango chake huku Chelsea wakiwa tayari kuingia katika mbio hizo pamoja na Liverpool kumsajili mshambuliaji huyo ambaye amemaliza msimu akiwa amefunga mabao tisa katika mechi 10 za mwisho alizocheza.Wakati Benteke akikiri kuwa hadhani kama atakuwepo Villa msimu ujao lakini nyota huyo wa kimataifa wa Ubelgiji amesisitiza kuwa atajiunga katika klabu ambayo itamuhakikishia nafasi ya kucheza mara kwa mara.Akihojiwa na luninga ya Sky, Benteke amesema kwasasa anamuachia shughuli hiyo wakala wake kwani yeye ndio anafahamu kitu gani anataka.

LIVERPOOL YAMTOLEA MACHO MILNER.


KLABU ya Liverpool inajipanga kufanya mazungumzo na kiungo wa kimataifa wa Uingereza na klabu ya Manchester City James Milner wiki hii.Liverpool imeamua kuupa kipaumbele uhamisho wa kiungo huyo aiyemaliza mkataba wake City na wana uhakika wanaweza kuafikiana.Kama mambo yote yakienda sawa, Milner mwenye umri wa miaka 29 ambaye alihamia City akitokea Aston Villa mwaka 2010, atajiunga rasmi na Liverpool Julai mosi mwaka huu.Milner alianza soka lake kaika klabu ya nyumbani kwao ya Leeds United kabla ya pia kuitumikia Newcastle United kwa miaka minne.Akiwa City Milner amefanikiwa kunyakuwa taji la Ligi Kuu mara mbili na moja la FA katika kipindi cha miaka mitano aliyokuapo hapo.