MENEJA wa Barcelona, Luis Enrique amesema anataka Pedro abakiye ndani Camp Nou kufuatia taarifa za kuwaniwa na Manchester United. Inaripotiwa kuwa United wanajipanga kutoa kitita cha paundi milioni 22 kwa mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, lakini Enrique amesisitiza hataki kabisa mchezaji huyo kuondoka. Akihojiwa Enrique aliwaambia wanahabari kuwa Pedro ni mchezaji wa kiwango cha juu na kama kocha anataka aendelee kubakia lakini hilo litakuwa ni uamuzi wake. Kocha huyo aliendelea kudai kuwa mchezaji yeyote anayetaka kuondoka ataruhusiwa lakini kwasasa hakuna taarifa kama hizo.
Tuesday, August 4, 2015
RAFAEL APEWA MIAKA MINNE LYON.
BEKI wa Manchester United, Rafael da Silva anatarajiwa kujiunga na Lyon ya Ufaransa kwa mkataba wa miaka minne. Rafael mwenye umri wa miaka 25 ambaye amefanikiwa kuitwa mara mbili katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil, alihamia United sambamba na pacha wake Fabio wakitokea klabu ya Fluminense mwaka 2008. Hata hivyo, Rafael ameshindwa kupata nafasi United ikiwa chini Louis van Gaal baada ya kuanza katika mechi sita pekee za Ligi Kuu msimu uliopita. Beki huyo aliandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter akiwashukuru mashabiki wa United kwa upendo wao katika kipindi chote cha miaka nane alichokuwepo Old Trafford. Akiwa United Rafael amefanikiwa kushinda mataji matatu ya Ligi kuu, moja la Kombe la Ligi na lingine la Klabu Bingwa ya Dunia katika kipindi alichokuwepo hapo.
BOATENG AANZA MAZUNGUMZO NA SPORTING LISBON.
KIUNGO wa Schalke, Kevin-Prince Boateng anajipanga kuendelea kubakia Ulaya kufuatia kuthibitisha kuanza mazungumzo na klabu kongwe ya Ureno Sporting Lisbon. Boateng mwenye umri wa miaka 28, ameripotiwa kukataa ofa kutoka klabu kongwe ya Saudi Arabia Al-Ittihad wiki iliyopita ili kusubiri timu kutoka Ulaya ambayo itamuhitaji. Sporting Lisbon wanatajwa kuanza mazungumzo na nyota huyo wa kimataifa wa Ghana ambaye amebakisha mwaka mmoja katika mkataba wake na Schalke. Boateng ambaye pia amewahi kuichezea AC Milan anatarajiwa kuuzwa kwa kitita cha euro milioni tano.
PLATINI AZIDI KUUNGWA MKONO.
MCHEZAJI wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa, Luis Fernandez amemuunga mkono Michel Platini kugombea nafasi ya urais katika Shirikisho la Soka Duniani-FIFA. Platini mwenye umri wa miaka 60, alitangaza kuwa atasimama kugombea nafasi hiyo ambayo rais wa sasa Sepp Blatter anatarajia kuiachia katika uchaguzi utakaofanyika Februari mwakani. Na Fernandez ambaye amewahi kucheza soka na Platini katika timu ya taifa kwenye miaka ya themanini anaamini ataweza kuliongoza shirikisho hilo. Akihojiwa Fernandez amesema anamfahamu Platini na kama kifanikiwa kuchaguliwa atataka kutengeneza muendelezo na kuipeleka FIFA mbele kwa kutafuta majawabu ya matatizo lukuki yanayolikabili shirikisho hilo kwasasa.
BENITEZ AWAKOMALIA BALE NA BENZEMA.
MENEJA wa Real Madrid, Rafael Benitez hategemei washambuliaji Gareth Bale na Karim Benzema kuondoka katika klabu hiyo. Bale mwenye umri wa miaka 26 amekuwa akihusishwa na tetesi za kuhamia Manachester United huku Benzema mwenye umri wa miaka 27 akiwaniwa na Arsenal. Akihojiwa Benitez amesema hataki kuzungumzia lolote kuhusu ofa zilizotolewa kwa ajili ya wachezaji wake kwani anachofahamu yeye Bale na Benzema wataendelea kuwepo Santiago Bernabeu. Mustakabali wa Bale umeibuka tena kufuatia Angel Di Maria kukaribia kukamilisha uhamisho wake wa paundi milioni 44.5 kutoka United kwenda Paris Saint-Germain. Hata hivyo, Benitez aliongeza kuwa Bale ni mchezaji muhimu kwao na anajua anafurahia kuwepo Madrid.
USAJILI LIGI KUU WATUMIA PAUNDI MILIONI 500 MPAKA SASA.
KIASI cha paundi milioni 500 zimetumika kwenye usajili wa Ligi Kuu katika kipindi hiki cha kiangazi, pungufu ya paundi milioni 335 zilizotumika kiangazi mwaka jana huku zikiwa zimebaki wiki nne kabla ya dirisha la usajili halijafungwa. Uhamisho wa Raheem Sterling kutoka Liverpool kwenda Manchester City kwa kitita cha paundi milioni 44 ndio usajili mkubwa kufanywa mpaka sasa. Meneja wa Manachester United Louis van Gaal amedokeza kufanya usajili wa kushangaza pamoja na kutumia paundi milioni 83 mpaka sasa. Kuanzia msimu wa 2016-2017 haki za matangazo ya kuonyesha mechi za Ligi Kuu imepanda kutoka paundi bilioni 3.018 mpaka paundi bilioni 5.136 kwa msimu mitatu. Kupata huko kwa mapato hayo kunafanya klabu itakayoburuta mkia katika Ligi Kuu kukunja kitita cha paundi milioni 99 kwa msimu huku bingwa akipata zaidi ya paundi milioni 150.
Monday, August 3, 2015
JEZI MPYA ZA MAN UNITED ZAZUA SONGOMBINGO.
KAMPUNI kongwe ya vifaa vya michezo ya Adidas imetetea aina ya jezi mpya walizotoa kwa ajili ya timu ya wanawake ya Manchester United baada ya kukosolewa vikali kutokana na jinsi ilivyotengenezwa. Kampuni hiyo ya Ujerumani Julai mwaka jana walisaini mkataba wa miaka 10 wenye thamani ya paundi milioni 750 wakichukua nafasi ya kampuni ya Nike iliyomaliza muda wake. Lakini wakati wakitambulisha jezi mpya zitakazotumika kwa ajili ya msimu ujao wa 2015-2016, jezi za wanawake ambazo zenyewe zimewekewa shingo pana kulinganisha na wanaume zimekosolewa vikali na wadau mbalimbali wakidai zinaacha sehemu kubwa ya kifua nje. Lakini msemaji wa Adidas amesisitiza katika taarifa yao kuwa jezi hizo zimetengenezwa baada ya kupata ushauri kutoka kwa mashabiki huku asilimia 75 wakiunga mkono aina hiyo ya fulana.
Subscribe to:
Posts (Atom)






