Thursday, August 4, 2016

CITY WANASA SAINI YA "NEYMAR AJAYE".

KLABU ya Manchester City imefanikiwa kumsajili winga chipukizi wa Brazil Gabriel Jesus kutoka klabu ya Palmeiras kwa ada ya paundi milioni 27. Jesus mwenye umri wa miaka 19 amekubali mkataba wa miaka mitano lakini ataendelea kubakia Palmeiras mpaka msimu wa soka wa Brazil utakapomalizika Desemba mwaka huu. Chipukizi huyo ambaye pia alikuwa akiwindwa na Barcelona, alipigiwa kura ya kuwa mchezaji bora anayechipukia nchini Brazil msimu uliopita na yupo katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil kinachoshiriki michuano ya Olimpiki. Jesus amefunga mabao 26 katika mechi 67 za kikosi cha alizocheza akiwa na Palmeiras na ndio anaongoza kwa ufungaji katika Ligi Kuu ya nchi hiyo kwasasa. City chini ya meneja mpya Pep Guardiola sasa wanakuwa wametumia kiasi cha paundi milioni 100 katika kipindi hiki cha kiangazi kwa kusajili wachezaji sita ambapo mbali na Jesus tayari wameshwasajili Leroy Sane, Ilkay Gundogan, Nolito, Oleksandr Zinchenko na Aaron Mooy.

MARTINEZ AWATAKA UBELGIJI KUBADILIKA.

ROBERTO Martinez amefurahi kuteuliwa kama kocha mpya wa timu ya taifa ya Ubelgiji lakini ameonya ni lazima wabadilike kama wanataka kushinda chochote. Ubelgiji walikuwa wakipewa nafasi kubwa katika michuano ya Ulaya mwaka huu lakini waliondolewa katika hatua ya robo fainali kwa kuondolewa na Wales. Kutokana na kufanya vibaya katika michuano hiyo waliamua kuachana na kocha Marc Wilmots na badala yake sasa wamemteua Martinez. Akihojiwa mara baad ya uteuzi huo, Martinez amesema ni heshima kubwa amepewa lakini kuna kazi kubwa ya kufanya pamoja na nchi hiyo kuwa na kikosi kizuri. Martinez aliendelea kudai kuwa nchi hiyo imejaaliwa vipaji lakini maandalizi ni muhimu hivyo anatarajia kukutana na kila mchezaji ili kuzungumza nao na kuwakumbusha majukumu yao kwa taifa. Kibarua cha kwanza cha Martinez akiwa kocha wa nchi hiyo utakuwa ni mchezo dhidi ya Hispania Septemba mosi mwaka huu jijini Brussels.

Wednesday, August 3, 2016

KLOPP ADOKEZA USAJILI ZAIDI.

MENEJA wa Liverpool, Jurgen Klopp anafikiria kutumia kipindi hiki cha usajili ili kuziba mapengo ya majeruhi walioanza kujitokeza katika kikosi chake hivi sasa. Meneja huyo raia wa Ujerumani atawakosa Mamadou Sakho, Joe Gomez na Lucas Leiva mwanzoni mwa msimu wa Ligi Kuu ambapo Liverpool inakabiliwa na mchezo mgumu dhidi ya Arsenal Agosti 14 mwaka huu. Upande wa beki wa kushoto ndio eneo ambalo Liverpool inaweza kuliimarisha zaidi katika dirisha hili la usajili kabla ya halijafungwa mwishoni mwa mwezi huu. Akihojiwa kuhusiana na suala la usajili Klopp amesema anadhani bado kuna maeneo katika kikosi chake yanahitaji kuzibwa kutokana na wachezaji kupata majeruhi na kukosa wachezaji wa kutosha kuziba nafasi hizo.

DRAXLER ABAINISHA KUTAKA KUONDOKA WOLFSBURG.

KIUNGO wa kimataifa wa Ujerumani, Julian Draxler amebainisha kuwa anataka kuondoka VfL Wolfsburg kwenda klabu kubwa kiangazi hiki na kuongeza tayari alishaweka wazi nia yake hiyo wakati wa michuano ya Ulaya. Draxler mwenye umri wa miaka 22 alitoa kauli hiyo wakati akifanyiwa mahojiano na jarida la Bild, akijibu madai ya meneja Dieter Hecking aliyedai kuwa kiungo huyo hawezi kuondoka klabuni kiangazi hiki. Akihojiwa Hecking alidai kuwa hawezi kujibu tetesi zote lakini anachofahamu yeye ni kuwa Draxler ataendelea kubaki nao kwa ajili ya msimu ujao. Hata hivyo, Draxler ambaye alijiunga na Wolfsbuef akitokea Schalke kwa euro milioni 34 mwaka 2014 na kusaini mkataba wa miaka mitano, amekanusha madai hayo akidai walipaswa kuzungumza naye kwanza kabla ya kutoa kauli hiyo hadharani. Draxler amecheza mechi 35 za mashindano yote msimu uliopita na kufunga mabao tisa na kusaidia mengine nane.

ZIDANE AMTAKA RODRIGUEZ ABAKI.

MENEJA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesisitiza kuwa anataka James Rodriguez abakie katika kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao. Rodriguez amekuwa akihusishwa na tetesi za kuondoka Madrid baada ya kuonekana kutokuwa katika mipango ya Zidane. Akihojiwa Zidane amesema kuna wachezaji wengi wanaocheza katika nafasi yake hivyo kunafanya uchaguzi wake kuwa mgumu. Hata hivyo, meneja huyo aliendelea kudai kuwa atakaa chini Rodriguez pindi atakaporejea kwani bado anamuhitaji katika kikosi chake.

CONTE KUMPA "SHAVU" N'GOLO KANTE IJUMAA.

MENEJA wa Chelsea, Antonio Conte amebainisha kuwa mchezaji mpya aliyesajiliwa kiangazi hiki N’Golo Kante atacheza walau kwa dakika 30 katika mchezo wa kirafiki wa Kombe la Kimataifa dhidi ya Chelsea Ijumaa hii. Kante amesajili na Chelsea kwa kitita cha paundi milioni 32 akitokea kwa mabingwa wa Ligi Kuu Leicester City lakini alikuwa bado hajacheza mechi yoyote kwa klabu yake hiyo mpya kufuatia kupewa mapumziko baada ya michuano ya Ulaya. Akihojiwa mara baada ya mazoezi ya kikosi chake yaliyofanyika katika Uwanja wa US Bank huko Minneapolis, Marekani, Conte amesema Kante amekuja akiwa katika hali nzuri na anatarajiwa kumtumia hata kwa kipindi kifupi katika mchezo wao wa Ijumaa. Beki huyo mwenye umri wa miaka 25 ni usajili wa pili wa Chelsea kufanya baada ya kumnasa Michy Batshuayi kutoka Marseille kwa kitita cha paundi milioni 33.

SCHALKE YANASA BEKI LA SEVILLA.

KLABU ya Schalke imekubali kumsajili beki wa kulia wa Sevilla Coke kwa mkataba wa miaka mitatu. Beki huyo mwenye umri wa miaka 29 ameichezea Sevilla kwa kipindi cha miaka mitatu baada ya kujiunga nao akitokea Rayo Vallecano mwaka 2011 na alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 3-1 waliopata dhidi ya Liverpool katika fainali ya Europa League mei mwaka huu. Coke pia alikuwepo katika kikosi cha Sevilla kilichotwaa mataji ya Europa League kwa miaka miwili mfululizo akifunga katika bao kwa chamoto ya mikwaju ya penati katika fainali ya mwaka 2014 dhidi ya Benfica. Mkurugenzi wa michezo wa Schalke Christian Heidel alithibitisha taarifa kumnasa Coke na kudai kuwa atakuwa msaada mkubwa katika safu yao ya ulinzi msimu ujao.