Tuesday, November 1, 2016

KLOSE ASTAAFU RASMI SOKA.

NGULI wa soka wa Ujerumani, Miroslav Klose ameamua kutundika daruga zake rasmi na kujiandaa kwa ajili ya kufanya kazi ya ukocha. Klose ambaye alistaafu soka la kimataifa baada ya kushinda Kombe la Dunia mwaka 2014, amekuwa bila klabu baada ya kuondoka Lazio majira ya kiangazi. Nguli huyo mwenye umri wa miaka 38, pia amecheza katika klabu za Fc Homberg, Kaiserslautern, Werder Bremen na Bayern Munich. Klose anaondoka akiwa ndio mfungaji wa wakati wote wa Ujerumani baada ya kufunga mabao 71 katika mechi 137 alizocheza. Chama cha Soka cha Ujerumani-DFB kilithibitisha taarifa hizo mapema leo na kuongeza kuwa sasa nguli huyo anakwenda kutafuta leseni ya ukocha.

INTER YAMTIMUA DE BOER.

KLABU ya Inter Milan imemtimua meneja wake Frank de Boer baada ya kushika nafasi hiyo kwa siku 85 pekee. Inter inashikilia nafasi ya 15 katika msimamo wa Serie A baada ya kutandikwa bao 1-0 na Sampdoria juzi, ikiwa ni kipigo chao cha nne katika mechi tano zilizopita. De Boer mwenye umri wa miaka 46, ambaye aliwahi kuwa beki wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, alikuwa akihusishwa na tetesi za kuwindwa na klabu za Uingereza majira ya kiangazi ikiwemo Everton na Southampton. De Boer alisaini mkataba wa miaka mitatu na Inter Agosti mwaka huu akichukua nafasi ya meneja wa zamani wa Manchester City Roberto Mancini. Hatua ya kutimuliwa kwa De Boer inakuja huku wakikabiliwa na mchezo wa Europa League Alhamisi hii dhidi ya Southampton.

FIFA YATUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KUFUATIA KIFO CHA MBUNIFU WA KOMBE LA DUNIA.

RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Gianni Infantino amesema milele soka litamshukuru mbunifu wa Kombe la Dunia Silvio Gazzaniga, ambaye amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95. Mbunifu huyo Muitaliano alifariki dunia nyumbani kwake katika jiji la Milan jana, huku mwanae wa kiume Giorgio akidai kuwa baba yake alifariki akiwa usingizini. Gazzaniga ambaye alikuwa mmoja wa wabunifu aliyejizolewa umaarufu mkubwa nchini Italia na dunia kote kwa miongo kadhaa, ndiye aliyesaidia kubuni aina mbalimbali na makombe ya soka likiwemo lile la UEFA Cup na UEFA Super Cup. Nguli huyo anakumbukwa zaidi kwa ubunifu wake wa Kombe la Dunia linalotumika hivi sasa ambalo lilichukua nafasi ya lile la Jules Rimet ambalo walizawadiwa Brazil moja kwa moja mwaka 1970.

AKADEMI YA REAL MADRID YAIPIGA BAO ILE YA BARCELONA.

JARIDA la Uchunguzi wa Soka la CIES limetoa orodha ya mwaka ya vituo vya akademi vilivyozalisha na Los Blancos ndio kimeibuka kidedea katika tano bora kwa kutoa wachezaji wengi zaidi. Kituo hicho cha Real Madrid kimetoa wachezaji 41 na kuwazidi mahasimu wao Barcelona waliopo nafasi ya pili kwa kutoa wachezaji 37 huku Manchester United wakikamilisha tatu bora kwa kutoa wachezaji 34. Klabu za Hispania zipo 11 katika orodha ya vilabu 50, huku klabu nne zikiwepo katika 10 bora lakini klabu za Ufaransa zenyewe zimeingia katika orodha ya 16 bora. Mbali na United klabu zingine za Uingereza zilizopo katika orodha hiyo ni pamoja na Arsenal, Tottenham Hotspurs, Southampton, Chelsea na Manchester City.

SPURS YAMTAKA ISCO KWA MKOPO.

KLABU ya Tottenham Hotspurs inadaiwa kutaka kumuwania kwa mkopo kiungo wa Real Madrid Isco katika dirisha dogo la usajili Januari mwakani. Spurs walituma maombi kama hayo kwa maofisa wa Madrid mwishoni kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili wa kiangazi lakini maombi yao yalikataliwa. Hata hivyo, Isco kwasasa ndio kwanza ameanza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara katika kikosi cha kwanza cha meneja Zinedine Zidane ila bado hajapewa ofa yeyote ya mkataba mpya kufuatia ule wa sasa kubakia miezi 18. Spurs wanaamini suala hilo linaweza kuwapa mwanya kwa kumnasa kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 lakini wanaweza kukabiliwa na changamoto kutoka kwa Chelsea kwa nao wanadaiwa kumuwania.

INTER KUMTENGEA VERRATTI ZAIDI YA MILIONI 50.

KLABU ya Inter Milan inadaiwa kuwa tayari kutenga kitita cha paundi milioni 58 kwa ajili ya kumnasa kiungo wa Paris Saint-Germain Marco Verratti. Taarifa juu ya uwezekano wa kutokuwa na maelewano kati ya Verratti na meneja mpya wa PSG Unai Emery, imezifanya klabu nyingi kubwa Ulaya kuangalia uwezekano wa kumsajili. Juventus, Arsenal na Chelsea ni miongoni mwa vilabu vinavyotajwa kumuwania lakini Inter wanadaiwa kuwa tayari kutoa fedha nyingi ili kushindania saini ya kiungo huyo.Kwasasa Inter wana fedha za kutosha za kutumia baada ya kununuliwa na kampuni ya China majira ya kiangazi na wanaweza kuanza kutumia fedha zao hizo katika usajili wa Januari.

MCHEZO DHIDI YA BARCELONA NI KAMA FAINALI - GUARDIOLA.

MENEJA wa Manchester City, Pep Guardiola amesema mchezo wao wa nyumbani wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Barcelona unapaswa kuchukuliwa kama fainali. City walipoteza mchezo wa kwanza kwa kutandikwa mabao 4-0 huko Hispania na kwasasa wanshika nafasi ya pili katika kundi C. Mshambuliaji Sergio Aguero anategemewa kuanza katika mchezo huo wa baadae leo sambamba na beki wa kulia Pablo Zabaleta. Akihojiwa Guardiola amesema walipoteza alama mbili dhidi ya Celtic hivyo wanapaswa kukusanya alama hizo kwa kuhakikisha wanashinda mchezo wao wa leo. Meneja huyo aliendelea kudai kuwa kwa upande wa Barcelona unaweza usiwe mchezo muhimu sana lakini kwao ni kama fainali.