
Friday, January 13, 2012
RIVALDO KUTIMKIA ANGOLA.
MCHEZAJI nyota wa zamani wa Brazil Rivaldo amethibitisha kuwa yuko njiani kujiunga na klabu ya Kabuscorp inayoshiriki Ligi Kuu nchini Angola. Rivaldo mwenye umri wa miaka 39 aliachwa na klabu ya nchini kwao ya Sao Paulo baada ya kuitumikia kwa muda wa miezi 12 tu lakini mwenyewe bado anapenda kucheza soka mpaka mwishoni mwa mwaka huu. Mchezaji huyo anayecheza nafasi ya kiungo tayari ameshashinda mataji mengi katika kipindi chake cha uchezaji soka ikiwemo Kombe la Dunia mwaka 2002, Klabu Bingwa ya Ulaya akiwa na AC Milan mwaka 2003 na tuzo ya mchezaji bora wa Dunia na Ulaya mwaka 1999. Akithibisha habari hizo Rivaldo amesema ni kweli yuko katika mazungumzo na klabu hiyo na anatarajia kusafiri kuelekea huko kuangalia kama wanaweza kufikia makubaliano.
GAUCHO ATISHIA KUIKACHA FLAMENGO.
Mshambuliaji wa kimataifa wa Brazil Ronaldinho Gaucho ametishia kuikacha klabu yake ya Flamengo kama hawatamlipa mshahara wake unaofikia kiasi cha dola milioni mbili. Katika taarifa iliyotolewa na wakala wake ambaye pia ni kaka yake Roberto de Assis imesema kuwa wanataka kufikia makubaliano kuhusu suala hilo ili Ronaldinho aweze kushiriki michuano ya Klabu Bingwa ya Amerika Kusini maarufu kama Copa Libertadores. Robo tatu ya mshahara wa mchezaji huyo inalipwa na Kampuni ya Masoko ya Traffic ambao hawajalipa kwa muda wa miezi mitano sasa kiasi kinachofikia dola milioni mbili na zaidi. De Assis alionya kuwa kama mchezaji huyo ambaye ana umri wa miaka 31 hatalipwa fedha hizo haraka atakubali moja ya maombi kutoka katika timu za aidha Italia, Hispania au Amerika Kusini zinazomuwania mshambuliaji huyo.
SUDAN YATAJA SILAHA ZAKE.
Sudan imetaja kikosi cha wachezaji 23 ambacho kitashiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika inayotarajiwa kuanza Januari 21 mpaka Februari 12 mwaka huu. Sudan ambayo imepangwa katika kubdi B kwenye michuano hiyo sambamba na timu za Angola, Burkina Faso pamoja na Ivory Coast. Katika kikosi hicho kutakuwa makipa Bahaeldin Abdallah, Mahjoub El Moez na Akram El Hadi Salem, mabeki watakuwa Nagmaldien Abdullah Ahmed Al Basha, Mowaia Bashir, Saifeldin Ali Idris, Bala Jaber, Ahmed Khalifa na Musab Omar. Wengine ni viungo Yousef Alaeldin, Mohamed Al Tahir, Ahmed Bashir, Badreldin El Doud, Nazir Hamed, Amir Kamal, Haitham Mostafa, Faisal Musa na Mohammed Mussi wakati washambuliaji watakuwa Ramadan Alagab, Abdulrahman Hassan, Mohammed Sheikh Eldin na Mudather Tayeb.
GERRARD AJIPIGA KITANZI CHA MUDA MREFU NA LIVERPOOL.
Nahodha wa klabu ya Liverpool Steven Gerrard amethibitisha kuwa amesaini mkataba mpya na mrefu na klabu hiyo ambao utamuweka hapo mpaka hapo atakapotundika daruga. Hatahivyo sio klabu hiyo wala Gerrard mwenyewe aliyesema mkataba huo utakuwa ni wa muda gani. Kiungo huyo wa kimataifa wa Uingereza ambaye alianza kuichezea klabu hiyo akiwa na miaka 18 Novemba mwaka 1998 ameshacheza mechi 566 na klabu hiyo na ameshinda mabao 144 likiwemo la penati alilofunga Jumatano dhidi ya Manchester City katika nusu fainali ya kwanza ya Kombe la Ligi. Mchezaji huyo pia ameichezea timu ya taifa ya Uingereza mara 89 na kushinda mabao 19. Gerrard ameisaidia klabu hiyo kushinda vikombe viwili FA pamoja na Kombe la Ligi mara mbili na kimoja cha Klabu Bingwa ya Ulaya lakini mchezaji huyo anasikitika kutokushinda kombe la Ligi Kuu ya nchi hiyo katika kipindi chote ambacho ameichezea klabu hiyo.
Thursday, January 12, 2012
INTERPOL KUWASHUGHULIKIA WATAKAOUZA MECHI UEFA 2012.
SHIRIKISHO la Soka barani Ulaya-UEFA na Polisi wa Kimataifa-Interpol wanaungana kwa pamoja kupambana na tabia za upangaji wa matokeo pamoja na vurugu zinazoweza kutokea uwanjani. Interpol wamekubaliana kufanya kazi pamoja na UEFA kwa kupeleka askari wake katika michuano ya Ulaya itakayofanyika Poland na Ukraine baadae mwaka huu. Rais wa UEFA Michel Platin alithibitisha kukutana na Katibu Mkuu wa Interpol Ronald Noble Jumatano na wanatarajia kusaini mkataba wa makubaliano hayo mapema. Interpol tayari imejitolea kusaidia vyama vya soka na suala la upangaji wa matokeo ambapo wameshasaini makubaliano ya miaka 10 na Shirikisho la Soka la Dunia mwaka uliopita kufungua kituo nchini Singapore kuwafundisha wachezaji pamoja na waamuzi kuepuka rushwa katika michezo.
PIRES KUMFUATA ANELKA.
KIUNGO wa zamani wa kimataifa wa Ufaransa na klabu ya Arsenal Robert Pires ameeleza kuwa ana matumaini ya kufuata nyayo za mchezaji mwenzie Nicolas Anelka kwenda kumalizia soka lake katika Ligi Kuu nchini China. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 38 yuko huru baada ya kuondoka Aston Villa mwezi may mwaka jana na aliliambia gazeti moja nchini Ufaransa kuwa ana mpango wa kumalizia soka lake katika bara la Asia kwenye kati ya China au hata India. Pires amesema kwasasa yuko katika mazungumzo ya mwanzo na baadhi ya timu huko China lakini pia ameshapata mawasiliano na India hivyo ataangalia wapi atakapokwenda kutegemeana na makubaliano watakayofikia. Hivi karibuni kuna tetesi zilisema kuwa mchezaji hhuyo kuna uwezekano mkubwa wa kurejea katika klabu ya Arsenal baada ya Thierry Henry kutua katika klabu hiyo kwa mkopo wa miezi miwili ila mwenyewe alikanusha tetesi hizo akidai hana mpango huo.
TOTTENHAM YAENDELEA KUJIZATITI EPL.
TIMU ya Tottenham Hotspurs imeendelea kufukuzia taji la Ligi kuu nchini uingereza ambalo kwa mara ya mwisho walilitwaa mwaka 1961 kwa kuifunga Everton mabao 2-0 jana usiku. Ushindi huo waliopata umewafanya wajizatiti katika nafasi ya tatu mwa msimamo wa ligi hiyo huku wakiwa wamefungana pointi na Manchester United wanakamata nafasi ya pili na kubakisha pointi tatu tu kuwafikia vinara wa ligi hiyo Manchester City. Mabao yaliyopatika katika kila kipindi cha mchezo huo kutoka kwa Aaron Lennon na Benoit Assou-Ekotto yaliisaidia timu hiyo inayotoka kaskazini mwa London kufikisha pointi 45 katika michezo 20 waliyocheza. Meneja wa Spurs Harry Redknapp amesema baada ya mchezo huo kuwa pamoja na bado mashabiki hawatakiwi kuota ndoto za kushinda taji hilo kwakuwa bado kuna michezo 18 mbele yao na huwezi kujua kitu gani kinaweza kutokea huko mbeleni.
Subscribe to:
Posts (Atom)