MKURUGENZI wa michezo wa Wolfsburg, Klaus Allofs amedai kuwa Julian Draxler atabakia katika klabu hiyo kipindi hiki cha kiangazi. Taarifa kutoka Ujerumani zilikuwa zikidai kuwa Wolfsburg walikuwa wako tayari kuuza zaidi ya wachezaji 10 katika kipindi hiki cha usajili na kuna uwezekano wa kuvutiwa na ofa ya euro milioni 60 kwa ajili ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 22. Wolfsburg walimaliza katika nafasi ya nane katika msimamo wa Bundesliga msimu uliopita na klabu hiyo tayari imekiri kuwa Andre Schurrle anaweza kuondoka kufuatia kuwindwa na Borussia Dortmund. Lakini Allofs amesema Draxler hatakuwa mchezaji mojawapo atayeuzwa katika kipindi hiki cha kiangazi.
Friday, July 15, 2016
BABU COSTA MGUU NJE MGUU NDANI CHELSEA.
MSHAMBULIAJI nyota wa Chelsea, Diego Costa anadaiwa kutaka kuondoka Stamford Bridge na kujiunga na Atletico Madrid. Taarifa zinadai kuwa klabu hiyo ya Ligi Kuu inafahamu nia ya mshambuliaji huyo na tayari wameshakataa ofa ya kwanza iliyotolewa na Atletico. Meneja mpya wa Chelsea Antonio Conte anatarajiwa kumshawishi Costa abakie katika klabu hiyo, kutokana na timu hiyo kushindwa kusajili mshambuliaji wa aina yake mpaka sasa. Costa amebakia kuwa chaguo la juu la Atletico na klabu hiyo ya Hispania inatarajiwa kutoa ofa nyingine kabla ya kufungwa kwa dirisha la majira ya kiangazi.
DORTMUND YAMVUTIA KASI GOTZE.
KLABU ya Borussia Dortmund imeendelea kukaa kimya juu ya tetesi za kiungo wa Bayern Munich, Mario Gotze kurejea katika timu yake hiyo ya zamani kipindi hiki cha kiangazi. Gotze mwenye umri wa miaka 24, alijiunga na Bayern akitokea Dortmund miaka mitatu iliyopita kwa kitita cha euro milioni 37. Hata hivyo, Gotze hajang’aa sana kama ilivyotegemewa toka alipotua Allianz Arena kwani amekuwa akihangaika kupata nafasi ya kucheza msimu uliopita kutokana na majeruhi ya mara kwa mara ambayo yamekuwa yakimuangama. Tetesi hizo zimedai kuwa Dortmund wako tayari kulipa euro milioni 23 na ofisa mkuu wake Hans-Joachim Watzke amekataa kukubali au kukataa uvumi huo unaozagaa.
NAPOLI YAKANUSHA TAARIFA HIGUAIN KWENDA JUVENTUS.
KLABU ya Napoli, imeponda vikali taarifa zilizozagaa kuwa wamekubali kumuuza Gonzalo Higuain kwa mahasimu wao wa Serie A Juventus. Nyota huyo wa kimataifa wa Argentina, amefunga mabao 36 katika Serie A msimu uliopita, ikiwa ni mabao 17 zaidi ya Maurizio Sarri ambaye alimaliza katika nafasi ya pili kwenye orodha hiyo. Arsenal walikuwa wakihusishwa na tetesi na kutaka kumsajili Higuain huku kukiwa na taarifa kuwa wanamjumuisha Olivier Giroud katika dili lao ili kuwashawishi Napoli wammuuze. Lakini ghafla zimezuka taarifa za mabingwa hao wa Serie A zikidai kuwa tayari wameshafikia makubaliano ya masuala binafsi na mchezaji huyo. Taarifa hizo zimekanushwa vikali na rais wa Napoli, Aurelio De Laurentiis ambaye amesisitiza taarifa hizo ni za kupuuza kwani hawana mpango wowote wa kumuuza nyota huyo.
KLUIVERT APEWA SHAVU PSG.
KLABU ya Paris Saint-Germain-PSG imetangaza kumteua mshambuliaji wa zamani wa kimataifa wa Uholanzi, Patrick Kluivert kuwa mkurugenzi mpya wa soka wa timu hiyo. Ujio wa Kluivert mwenye umri wa miaka 40 unakuja kufuatia kuteuliwa kwa Unai Emery kuwa kocha mkuu akichukua nafasi ya Laurent Blanc aliyeondoka mwezi uliopita. Taarifa ya PSG imedai kuwa Kluivert atashughulikia maendeleo ya soka ya klabu kitaifa na kimataifa huku akitengeneza mipango ya kimichezo ya muda mrefu. Akihojiwa baada ya kupata kibarua hicho, Kluivert amesema ni hesima kubwa kwake kujiunga na klabu kubwa kama PSG na kupewa majukumu mazito kama hayo. Kluivert aliendelea kudai kuwa lengo kubwa la klabu ni kusonga mbele na amepania kufanya hilo kwa weledi mkubwa.
Thursday, July 14, 2016
TANZANIA YAKWEA KWA NAFASI 13 VIWANGO FIFA.
TANZANIA imekwea kwa nafasi 13 mpaka kufikia nafasi ya 123 katika viwango vya ubora vipya vilivyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani-FIFA leo. Mwezi uliopita Tanzania ilikuwa katika nafasi ya 136 lakini mwezi huu imepanda na kushinda nafasi hiyo huku kwa upande wa Afrika ikishika nafasi ya 36 ikizizidi nchi za Burundi iliyopo nafasi ya 125 duniani na 38 Afrika na Sudan Kusini nafasi ya 153 kwa 47 kwa nchi ukanda wa Afrika Mashariki. Nchi inayoongoza kwa ukanda wa Afrika Mashariki ni Uganda waliopo nafasi ya 69 duniani na 15 Afrika wakifuatiwa na Kenya waliopo nafasi ya 86 duniani na 22 Afrika na Rwanda ndio wanaoshika nafasi ya tatu wakiwa katika nafasi ya 111 duniani na 32 Afrika. Kwa upande wa Afrika orodha hiyo bado imeendelea kushikiliwa na Algeria ambao wako nafasi ya 32 duniani wakifuatiwa na Ivory Coast katika nafasi ya 35, Ghana nafasi ya 36, Senegal nafasi ya 41 na Misri ndio anakamilisha tano bora ya Afrika wakiwa nafasi ya 43. Kwa upande wa orodha za jumla, Argentina bado wameendelea kukaa kileleni wakifuatiwa na Ubelgiji katika nafasi ya pili, Colombia nafasi ya tatu, Ujerumani nafasi ya nne, mabingwa wa Copa America Chile nafasi ya tano na mabingwa wa Ulaya Ureno wao wako nafasi ya sita.
SANCHEZ AMPA WENGER MCHECHETO.
KLABU ya Arsenal inahaha kuhakikisha Alexis Sanchez anakuwa fiti kabla ya mechi yao ya ufunguzi ya msimu mpya wa Ligi Kuu baadae mwezi ujao. Sanchez alipata majeruhi ya kifundo cha mguu wakati wa michuano ya Copa America na amekuwa akipatiwa matibabu katika kipindi hiki cha mapumziko ya kiangazi. Arsenal wamekuwa akifuatilia kwa karibu maendeleo ya nyota wao huyo na kuna hofu anaweza kukosa mwanzo wa msimu ambapo timu hiyo hiyo itaikaribisha Liverpool katika Uwanja wa Emirates Agosti 14 mwaka huu. Meneja wa Arsenal, Arsene Wenger atataka Sanchez awe fiti ka ajili ya mchezo huo haswa kutokana na uhaba wa washambuliaji alionao kutokana na michuano ya Ulaya iliyomalizika hivi karibuni. Kutokana na michuano hiyo Olivier Giroud, Mesut Ozil na Aaron Ramsey hawatajiunga na wenzao kwa mazoezi ya maandalizi msimu mpaka Agosti 8 ikiwa ni siku saba kabla ya mchezo dhidi ya Liverpool.
Subscribe to:
Posts (Atom)






