Thursday, October 20, 2011

WAMILIKI WA VILABU KUU UINGEREZA WAANZISHA MGOGORO.


VILABU kadhaa vinavyocheza katika ligi kuu ya Premier vimekuwa na mapendekezo ya kutaka utaratibu wa timu kuteremshwa daraja kukomeshwa.

Hayo ni kwa mujibu wa mkurugenzi mkuu wa chama cha meneja wa timu za soka nchini Uingereza, (LMA), Richard Bevan.

Manchester City ni kati ya vilabu vinavyomilikiwa na wageni.

Bevan anahofia kwamba ikiwa vilabu zaidi vitauziwa wawekezaji wa kigeni, basi huenda wakapata nguvu zaidi katika kutekeleza mabadiliko hayo.

Lakini wanaosimamia ligi kuu ya Premier wamesema timu kushuka daraja, na nyingine kupanda, ni kati ya hatua ambazo huifanya ligi kuu kuwa ya kuvutia.

Bevan vile vile anatumaini kwamba kamati ya bunge inayochunguza usimamizi wa soka itaweza kuzuia pendekezo hilo hatimaye kutekelezwa.

"Tuna matumaini mno kwamba ripoti hiyo itafanikiwa katika kukisaidia chama cha soka cha FA kuanzisha utaratibu wa kutoa leseni kwa vilabu," alielezea.

"Hii ni kwa kuwa baadhi ya vilabu vinavyomilikiwa na wageni wameanza kuzungumza juu ya namna ya kuepuka kushuka daraja katika ligi kuu ya Premier.

"Ikiwa tutakuwa na wamiliki wengine wanne au watano hivi, hayo huenda yakafanyika."

No comments:

Post a Comment