Wednesday, November 2, 2011

WENGER AKIRI ALIKOSEA KUTOMWANZISHA VAN PERSIE.



Arsene Wenger amekiri "alibahatisha" kutomuanzisha tangu mwanzo Robin van Persie wakati Arsenal ilipopambana na Marseille katika Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.Mshambuliaji Van Persie, aliingia kipindi cha pili wakati Gunners ilipolazimishwa sare ya 0-0 dhidi ya Marseille katika uwanja wao wa Emirates.Meneja wa Arsenal Wenger amesema: "Ilikuwa ni bahati nasibu unaweza kusema lakini alikuwa amechoka sana baada ya mechi ya Jumamosi dhidi ya Chelsea."Unajua tunacheza mechi 50 kwa mwaka - hawezi kucheza mechi 50." Van Persie aliingia dakika ya 62 na nusura angefunga bao baada ya kutanguliziwa pasi ndefu na Tomas Rosicky, lakini alishindwa jaribio lake la kuubetua mpira dhidi ya mlinda mlango Steve Mandanda, ambaye aliunyaka mpira huo kwa urahisi."Alipata nafasi na angefunga, basi ingekuwa safi sana," alisema Wenger. Van Persie alipumzishwa siku tatu baada ya kupachika mabao matatu peke yake wakati Arsenal ilipoilaza Chelsea mabao 5-3 na kuongeza hazina yake ya mabao kufikia 28 katika mechi 27 za ligi alizoichezea klabu hiyo.Wenger amekiri mpambano wa kukata na shoka wa Stamford Bridge uliwaacha wachezaji wake kadha kujihisi wamechoka.Mshambuliaji wa pembeni wa Arsenal Theo Walcott ameongeza: "Mechi ya Jumamosi ilituchosha lakini tulifahamu ambacho tulikuwa tukikitazamia katika Ligi ya Ubingwa wa Ulaya.
Licha ya kuonekana kuteleza, Arsenal inaendelea kushikilia usukani katika kundi lao, pointi moja nyuma ya Marseille wakiwa wamesaliwa na mechi mbili.Akizungumzia mchezo dhidi ya Marseille, Wenger amesema: "Tulilinda lango vyema, tulifanya kazi ya ziada lakini tulikosa ubora fulani dakika za mwisho". "Hatuna budi kuwapongeza Marseille, walihami lango lao vizuri sana na walituzuia kucheza mchezo wetu."

No comments:

Post a Comment