|
Wachezaji wa Chelsea wakishangilia bao la kusawazisha dhidi ya Manchester City. |
TIMU ya Chelsea imefanikiwa kumaliza ubabe wa Manchester City wa kutofungwa katika Ligi Kuu nchini Uingereza baada ya kufanikiwa kuifunga timu hiyo mabao 2-1 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Stamford Bridge. Chelsea ambao sasa wamerudi katika mbio za kusaka ubingwa wa ligi hiyo ilibidi wafanye kazi ya ziada baada ya mshambuliaji wa City Mario Balotelli kuipatia timu yake bao la kuongaza ikiwa ni dakika mbili toka mpira uanze. Bao halikuonyesha kuwakatisha tamaa Chelsea ambao walionyesha kutulia katika mchezo huo kusaka bao la kusawazisha na juhudi zao hizo zilizaa matunda dakika ya 34 ambapo mchezaji Raul Meireles aliisawazishia bao timu yake akimalizia pasi murua iliyopigwa na Bosingwa na kuzifanya timu hizo kwenda mapumziko zikiwa zimetoshana nguvu.
|
Kadi nyekundu aliyopewa Gael Clichy. |
Kipindi cha pili hakikwenda vizuri kwa upande wa City baada ya beki wake Gael Clichy kutolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kupewa kadi ya pili ya njano na kulazimika kucheza karibu dakika 30 zilizobakia wakiwa pungufu. Chelsea walitumia vyema mapungufu hayo na kuongeza kasi ya mashambulizi katika lango la City na juhudi zao hizo zilizaa matunda dakika nane kabla ya mpira kumalizika kwa kuzawadiwa penati iliyofungwa na Frank Lampard kufuatia beki wa City Joleon Lescott kuunawa mpira katika eneo la hatari.
No comments:
Post a Comment