Wednesday, December 7, 2011

UEFA CHAMPIONS LEAGUE: CHELSEA, MARSEILLE ZATINGA HATUA YA MTOANO.

TIMU ya Chelsea jana usiku ilikata tiketi ya kucheza hatua ya mtoano ya timu 16 ya michuano ya Klabu Bingwa Ulaya baada ya kufanikiwa kuigaragaza Valencia mabao 3-0 katika mchezo uliochezwa katika Uwanja wa Stamford Bridge. Mabao mawili yaliyofungwa na mshambuliaji wake Didier Drogba na moja la Ramires yaliiwezesha timu hiyo kumaliza wakiwa vinara wa kundi E ikifuatiwa na Bayer Leverkusen ambao wamemaliza wakiwa wa pili baada ya kutoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Genk. Katika mchezo mwingine uliokuwa mkali na wa kusisimua timu ya Marseille ilifanikiwa kuibanjua Borussia Dortmund kwa mabao 3-2 katika mchezo wa kundi F hivyo kupelekea timu hiyo kuungana na Arsenal ambao walifungwa na Olympicos mabao 3-1 katika hatua mtoano. Michezo mingine ya michuano hiyo inatarajiwa kupigwa tena leo ambapo vinara wanaoongoza Ligi Kuu nchini Uingereza Manchester City ina kibarua kizito cha kuhakikisha inaifunga Bayern Munich ili kujihakikishia nafasi ya kusonga mbele huku mahasimu wao Manchester United nao wakihitaji ushindi wowote dhidi ya Basle ili nao waweze kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment