Thursday, January 26, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

WARUNDI KUICHEZESHA SIMBA KIGALI 
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua waamuzi kutoka Burundi kuchezesha mechi ya Kombe la Shirikisho kati ya Simba ya Tanzania na Kiyovu Sport ya Rwanda itakayochezwa jijini Kigali. Waamuzi hao ni Thierry Nkurinziza atakayekuwa katikati wakati wasaidizi wake ni Jean-Claude Birumushahu na Jean-Marie Hakizimana. Mwamuzi wa akiba atakuwa Hudu Munyemana kutoka Rwanda. Kamishna wa mechi hiyo ni Abbas Sendyowa kutoka Uganda. Mechi hiyo namba 13 itachezwa Februari 18 mwaka huu kwenye Uwanja wa Amahoro jijini Kigali, na itaanza saa 9.30 kwa saa za Rwanda. Mechi ya marudiano itachezwa Machi 4 mwaka huu, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.



CAF YAMTEUA LIUNDA KUSIMAMIA MECHI
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Leslie Liunda wa Tanzania kuwa Kamishna wa mechi namba 3 ya Ligi ya Mabingwa kati ya AS Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) na Atletico Olympique ya Burundi itakayochezwa kati ya Februari 17, 18 na 19 mwaka huu jijini Kinshasa. Waamuzi wa mechi hiyo ambao wanatoka Gabon watakuwa Mbourou Roponat, Wilfred Nziengu na David Obamba. Mwamuzi wa akiba kutoka DRC ni Mupemba Nkongolo. Mechi ya marudiano kwa timu hizo itachezwa kati ya Machi 2, 3 na 4 jijini Bujumbura ambapo Kamishna atakuwa Eugene Katamban kutoka Uganda.



TAMASHA LA KUVUMBUA VIPAJI (GRASSROOT) DAR
Tamasha la mafunzo ya kuhamasisha watoto kucheza mpira wa miguu na kuvumbua vipaji (Grassroot) kwa shule maalum zilizochaguliwa katika Mkoa wa Dar es Salaam linaendelea Februari 3 mwaka huu. Siku hiyo tamasha hilo litafanyika katika Shule ya Msingi Mtoni Kijichi wilayani Temeke kuanzia saa 3 asubuhi hadi saa 6 mchana. Februari 10 mwaka huu tamasha lingine litafanyika katika Shule ya Msingi Kinyerezi wilayani Ilala. Watoto (wa kike na kiume) wanaotakiwa kushiriki katika matamasha hayo ambayo yataendelea kila wiki katika shule mbalimbali za Dar es Salaam hadi Agosti 24 mwaka huu ni wa kuanzia umri wa miaka 6 hadi 12. Matamasha hayo ni mwendelezo wa uzinduzi wa Grassroot katika tamasha (festival) kubwa lililofanyika Desemba 17 mwaka jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na watoto 1,200 baada ya semina iliyoendeshwa na Mkufunzi kutoka Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).

No comments:

Post a Comment