Monday, January 9, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF.

MECHI KUCHEZWA SIKU TATU KWA WIKI
Siku za mechi (match days) kwa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2011/2012 ambayo itaanza mzunguko wake wa pili Januari 21 mwaka huu sasa itakuwa ni Jumamosi, Jumapili na Jumatano tu. Uamuzi huo umefanya na Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) iliyokutana Januari 5 mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine ilikuwa kupitia ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom na ile ya Daraja la Kwanza. Kutokana na kituo cha Dar es Salaam kuwa na timu saba kati ya 14 za Ligi Kuu zinazotumia viwanja viwili tu (Uwanja wa Taifa na Uwanja wa Azam), kamati imepitisha uamuzi kuwa mechi mbili zinaweza kuchezwa kwa wakati mmoja (Taifa na Azam) ili ligi ichezwe ndani ya kalenda. Timu zinazotumia viwanja hivyo kama vya nyumbani katika Ligi Kuu ya Vodacom ni African Lyon, Azam, JKT Ruvu Stars, Moro United, Villa Squad, Simba na Yanga.

LIGI DARAJA LA KWANZA FEBRUARI 4
Mzunguko wa pili wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara inayochezwa katika makundi matatu tofauti kwa mtindo wa nyumbani na ugenini itaanza Februari 4 mwaka huu. Timu zitakazomaliza katika nafasi tatu za juu zitacheza hatua ya fainali itakayokuwa na timu tisa. Kundi A lenye timu za Burkina Faso ya Morogoro, Mgambo Shooting ya Tanga, Morani ya Manyara, Polisi ya Dar es Salaam, Temeke United ya Dar es Salaam na Transit Camp ya Dar es Salaam litaanza ligi hiyo kwa mechi moja kati ya Morani na Burkina Faso itakayochezwa mkoani Manyara. Februari 4 mwaka huu katika kundi B kutakuwa na mechi kati ya Small Kids ya Rukwa na Polisi ya Iringa itakayochezwa mjini Morogoro, Mbeya City na Tanzania Prisons zitaumana Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya wakati Majimaji na Mlale JKT wataoneshana kazi Uwanja wa Majimaji mjini Songea. Kundi C mechi za ufunguzi zitakuwa kati ya Manyoni FC na AFC itakayofanyika mjini Singida, Rhino FC dhidi ya Polisi ya Tabora zitacheza Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wakati 94 KJ na Polisi ya Morogoro zitakwaruzana Februari 5 mwaka huu mjini Mlandizi.

16 WAOMBA AJIRA YA OFISA WA LIGI
Mchakato wa kumpata Ofisa wa Ligi bado unaendelea. Kamati ya Ligi ilipitia maombi ya watu 16 yaliyowasilishwa TFF kwa nafasi ya Ofisa huyo kwa ajili ya Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza. Mwisho wa kutuma maombi ilikuwa Desemba 28 mwaka jana. Maombi yote 16 yalipitiwa ambapo waliopita katika mchujo huo wa kwanza wataitwa kwa ajili ya usaili. Waombaji wataarifiwa siku ya usaili kupitia mawasiliano waliyotumia wakati wanawasilisha maombi yao.

KANYENYE AREJESHEWA KIBENDERA FIFA
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) limemthibitisha tena mwamuzi msaidizi John Kanyenye wa Tanzania kuingia katika orodha yake kwa mwaka 2012. Awali FIFA ilituma TFF majina ya jumla ya waamuzi 14 wa Tanzania wakiwemo waamuzi wasaidizi wawili wapya kwa ajili ya mwaka 2012. Jina la Kanyenye halikuwamo katika orodha hiyo iliyokuwa imetumwa awali. Kwa vile Kanyenye alikuwamo katika orodha ya waamuzi wa Tanzania wanaotambuliwa na Shirikisho hilo kwa mwaka 2011 na jina lake halikurudi, TFF ililazimika kuiandikia FIFA ili kupata ufafanuzi wa kuenguliwa kwa Kanyenye. Uamuzi wa FIFA kumrejesha Kanyenye kwenye orodha inaifanya Tanzania sasa kuwa na jumla ya waamuzi 15. Waamuzi wa kati ni Israel Mujuni, Judith Gamba, Orden Mbaga, Ramadhan Ibada na Sheha Waziri. Waamuzi wasaidizi ni Ali Kinduli, Erasmo Clemence, Ferdinand Chacha, Hamisi Chang’walu, John Kanyenye, Josephat Bulali, Khamis Maswa, Mwanahija Makame, Saada Tibabimale na Samuel Mpenzu.

No comments:

Post a Comment