Thursday, February 23, 2012

GHANA KUMUANGUKIA BOATENG.

KOCHA wa timu ya taifa ya Ghana Goran Stevanovic amesema kuwa kiungo wa timu hiyo Kevin-Prince Boateng anatarajiwa kurejea katika kikosi hicho mapema. Kauli ya kocha huyo imekuja wakati akizungumza na waandishi wa habari waliomtaka kufafanua ni kitu gani kiliwatokea mpaka wakashindwa kufanya vyema katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika iliyofanyika Gabon na Guinea ya Ikweta. Kocha huyo aliendelea kusema kama ataendelea kukinoa kikosi hicho basi hana budi kuongeza damu change zaidi katika kikosi hicho akiwemo kiungo Boateng ambaye anakipiga katika timu ya AC Milan ya Italia. Stevanovic ambaye ni raia wa Serbia amesema kuwa jitihada za makusudi lazima zifanyike kumshawishi mchezaji huyo kurejea katika kikosi hicho maarufu kama Black Stars. Boateng aliandika barua kwa Shirikisho la Soka la Ghana-GFA kuomba kupumzika kuichezea Black Stars Novemba mwaka jana kwa kile alichodai matatizo ya kiafya yaliyokuwa yakimwandama.

No comments:

Post a Comment