Friday, February 17, 2012

SUNZU AZITAMANI CHELSEA NA BOLTON.

SHUJAA wa timu ya taifa ya Zambia Stoppila Sunzu anatamani kwenda Uingereza kucheza soka la kulipwa baada ya kufanikiwa kufunga penati ya mwisho dhidi ya Ivory Coast iliyoiwezesha timu yake kunyakuwa Kombe la Mataifa ya Afrika Jumapili iliyopita. Akihojiwa Sunzu ambaye ameshawahi kuichezea klabu ya Chateauroux ya nchini Ufaransa katika msimu wa mwaka 2008-2009 amesema kuwa anatamani kurudi kucheza soka ya kulipwa Ulaya. Sunzu aliendelea kusema kuwa ana ndoto za siku moja kucheza soka ya kulipwa nchini Uingereza haswa katika timu za Chelsea na Bolton Wanderers. Zambia ilifanikiwa kuwafunga Ivory Coast kwa changamoto ya mikwaju ya penati 8-7 jijini Libreville, Gabon baada ya kwenda sare ya bila kufungana katika muda wa kawaida na kufanikiwa kunyakuwa taji hilo kwa mara ya kwanza. Sunzu alishawahi kufanya majaribio nchini Uingereza katika klabu ya Reading baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika michuano ya Kombe la Dunia ya vijana chini ya miaka 20 iliyofanyika nchini Canada lakini alishindwa kupata kibali cha kufanya kazi nchini Uingereza.

No comments:

Post a Comment