Thursday, March 15, 2012

PELE KUWEPO MKUTANO WA USULUHISHI, FIFA NA SERIKALI YA BRAZIL.

NGULI wa soka wa zamani wa Brazil Pele anatarajiwa kujiunga na Rais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Sepp Blatter pamoja na rais wa nchi hiyo Dilma Rousseff katika mkutano wa usuluhishi unaotarajiwa kufanyika kesho. Blatter anatarajiwa kusafiri kuelekea Brasilia ambao ndio mji mkuu wa Brazil kujaribu kurekebisha tofauti baada ya Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke kuchafua hali ya hewa baada ya kutoa kauli kuhusu maandalizi ya nchi hiyo ya Kombe la Dunia ambayo iliwaudhi. Katika taarifa yake Blatter amesema kuwa anafurahishwa kuwepo kwa nguli huyo wa soka katika mkutano huo ambapo wanatarajia kuzungumzia pia sula la maandalizi na kitu gani kinahitajika kufanywa katika miezi hii michache ya maandalizi iliyobakia. Taarifa hiyo imekuja ikiwa ni siku mbili tu toka aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka la nchi hiyo Ricardo Teixeira kujiuzulu kutokana na matatizo ya kiafya, Pele alikuwa na uhusiano usiokuwa mzuri na Teixeira ambaye alishindwa hata kumualika katika droo ya kupanga timu zitakazowania tiketi ya kushiriki michuano ya Kombe la Dunia. Hatahivyo baadae Rousseff alimteua Pele kuwa balozi wa Kombe la Dunia wa nchi hiyo.

No comments:

Post a Comment