Friday, March 23, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

KUONA MORO UNITED, AFRICAN LYON 1,000/-
Viingilio kwenye mechi namba 149 ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kati ya Moro United na African Lyon itakayochezwa kesho (Machi 24 mwaka huu) Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam ni sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 kwa jukwaa kuu. Mwamuzi Hashim Abdallah wa Dar es Salaam ndiye atakayechezesha mechi hiyo akisaidiwa na Ephraim Ndissa na Abdallah Selega wakati mwamuzi wa akiba ni Oden Mbaga. Wote pia wanatoka Dar es Salaam. Kamishna wa mechi hiyo ni James Mhagama kutoka mkoani Ruvuma. Pia viingilio hivyo ndivyo vinavyotumika kwa mechi zote za Ligi Kuu ya Vodacom zinazochezwa Uwanja wa Chamazi zisizohusisha timu za Simba na Yanga. VPL itaendelea tena Machi 28 mwaka huu kwa mechi kati ya Ruvu Shooting Stars itakayocheza na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mabatini mjini Mlandizi wakati Moro United itakuwa mwenyeji wa Villa Squad katika mechi namba 153 itakayofanyika Uwanja wa Chamazi.

MMOJA AONGEZWA TWIGA STARS
Kocha Charles Boniface Mkwasa wa Twiga Stars amemuongeza mshambuliaji Rehema Salum wa Shule ya Sekondari Lord Baden ya mkoani Pwani kwenye kikosi hicho kitakachoingia kambini Machi 25 mwaka huu. Rehema aliibuka mfungaji bora kwenye mashindano maalumu ya Siku ya Wanawake Duniani yaliyoshirikisha shule nane za sekondari za Mkoa wa Dar es Salaam na kuhitimishwa Machi 8 mwaka huu. Twiga Stars itaingia kambini kwenye kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) iliyoko Ruvu mkoani Pwani ikiwa ni sehemu ya maandalizi kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Fainali za Wanawake Afrika (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini Equatorial Guinea. Timu hiyo itacheza na Ethiopia kusaka tiketi ya kwenda Equatorial Guinea ikianzia ugenini Addis Ababa kwa mechi itakayochezwa Mei 26 mwaka huu. Timu hizo zitarudiana wiki mbili baadaye jijini Dar es Salaam. Katika raundi ya kwanza, Twiga Stars iliitoa Namibia kwa jumla ya mabao 7-2. Ilishinda ugenini 2-0 na kuibuka na ushindi mnono nyumbani wa mabao 5-2. Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ili ishiriki vyema michuano ya AWC. Wachangiaji wa Twiga Stars wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389 ambapo kiwango cha juu kinachoweza kutumwa kwa muhamala (transaction) mmoja ni sh. 500,000. Katika uzinduzi huo, Waziri Dk. Mukangara alichangia sh. milioni moja.

MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI
Mtihani kwa kwa ajili ya watu wanaotaka kuwa mawakala wa wachezaji na mechi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Machi 31 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (FIFA). Kwa wanaotaka uwakala huo wanatakiwa kujisajili ambapo watapewa kanuni mbalimbali za FIFA na TFF ili waweze kujiandaa kikamilifu kwa mtihani huo utakaokuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ya mtihani huo ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka TFF.

No comments:

Post a Comment