Friday, March 30, 2012

TAARIFA MBALIMBALI KUTOKA TFF LEO.

LWIZA KUSIMAMIA EL MERREIKH, PLATINUM CL
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limemteua Alfred Kisongole Lwiza kuwa Kamishna wa mechiya Ligi ya Mabingwa (CL) kati ya El Merreikh ya Sudan na FC Platinum ya Zimbabwe. Mechi hiyo ya marudiano ya raundi ya kwanza itachezwa Aprili 7 mwaka huu kwenye Uwanja wa El Merreikh jijini Khartoum, Sudan kuanzia saa 2 kamili usiku. Katika mechi ya kwanza iliyochezwa wikiendi hii jijini Harare timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2. El Merreikh ni moja ya timu ambazo CAF iliziingiza moja kwa moja katika raundi ya kwanza. FC Platinum iliingia raundi ya kwanza baada ya kuing’oa Green Mamba ya Swaziland katika raundi ya awali.

ZIMBABWE YAITAKA TWIGA STARS
Chama cha Mpira wa Miguu Zimbabwe (ZIFA) kimeomba mechi ya kirafiki kati ya timu yake ya Taifa ya wanawake na Twiga Stars. Mechi hiyo itakayochezwa kati ya Aprili 28 au 29 mwaka huu jijini Harare. Mechi hiyo ni sehemu ya maandalizi ya timu ya Zimbabwe kwa ajili ya kutafuta tiketi ya kucheza Fainali zaNane za Kombe la Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika Novemba mwaka huu nchini EquatorialGuinea. Twiga Stars ambayo iko kambini mkoani Pwani tangu Machi 25 mwaka huu chini ya Kocha Charles Boniface Mkwasa nayo inajiwinda kwa fainali hizo ambapo itacheza mechi ya kwanza Mei 26 mwaka huu jijini Addis Ababa dhidi ya Ethiopia. Zimbabwe yenyewe inacheza na Senegal. Machi 10 mwaka huu, Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara alizindua akaunti ya Twiga Stars kupitia Tigo Pesa kuichangia timu hiyo ili ishiriki vyema michuano ya AWC. Wachangiaji wa Twiga Stars wanatakiwa kutuma mchango wao kwenda namba 13389 ambapo kiwango cha juu kinachoweza kutumwa kwa muhamala (transaction) mmoja ni sh. 500,000. Katika uzinduzi huo, Waziri Dk. Mukangara alichangia sh. milioni moja.

MTIHANI WA MAWAKALA WA WACHEZAJI
Mtihani kwa ajili ya mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Machi 31 mwaka huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa MiguuTanzania (FIFA). Watu watatu wamejitokeza kufanya mtihani huo utakaokuwa na sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka TFF.

SIMBA, YANGA ZASAKA POINTI VPL
Yanga na Simba ni miongoni mwa timu nne zitakazokuwa viwanjani kesho (Machi 31 mwaka huu) kusaka pointi tatu za Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) ambayo iko katika raundi ya 22. Uwanja wa Mkwakwani, jijini Tanga utakuwa mwenyeji wa mechi namba 148 kati ya Coastal Union na Yanga. Mechi hiyo itachezeshwa na mwamuzi Rashid Msangi wa Dodoma ambaye atasaidiwa na Rashid Lwena (Ruvuma) na Issa Malimali (Ruvuma). Mwamuzi Amon Paul wa Musoma ndiye atakayechezesha mechi namba 151 kati ya African Lyon na Simba itakayochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Viingilio kwenye mechi ya African Lyon na Simba ni sh. 3,000 kwa viti vya kijani na bluu, sh. 5,000 viti vya rangi ya chungwa, sh. 10,000 kwa VIP C na B wakati VIP A ni sh. 15,000. Aprili Mosi mwaka huu kutakuwa na mechi ya VPL kati ya Azam na Ruvu JKT itakayochezwa Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam. Kiingilio katika mechi hiyo kitakuwa sh. 1,000 kwa mzunguko na sh. 5,000 jukwaa kuu.

No comments:

Post a Comment