Tuesday, April 17, 2012

SILVA AVUNJIKA VIDOLE AKIPIGANA NA MASHABIKI.

MSHAMBULIAJI wa Boca Juniors, Santiago Silva ameungana na wachezaji wengine wa mabingwa hao wa zamani wa Argentina ambao ni majeruhi baada ya kuvunjika vidole vyake viwili kwa kupigana na mashabiki wa mahasimu wao katika Ligi Daraja la Kwanza timu ya Tigre. Taarifa kutoka vyombo vya habari vya nchi hiyo zinasema kuwa sakata hilo lilitokea wakati wachezaji wengine wakiingia kwenye basi ambapo mashabiki wa Tigre walipoanza kumtupia maneno ya kumdhalilisha mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Uruguay na kuzua tafrani baada ya Boca Juniors kufungwa mabao 2-1 na Tigre. Sakata hilo linaweza kusababisha klabu ya Boca Juniors kupewa adhabu kutokana na wachezaji wake kushindwa kujizuia katika vurugu hizo wakati Tigre wao wanaweza kupewa adhabu kwa kushindwa kuweka ulinzi wa polisi mahali ambapo basi la wachezaji wa Boca lilipaki. Huo ni mchezo wa kwanza kwa Boca Juniors kupoteza kati ya michezo 19 ambayo wamecheza ugenini wakati Tigre huo unakuwa ni ushindi wao wa kwanza katika michezo mitano waliyocheza hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment