DERRICK Walullya, beki wa kimataifa wa Uganda na mshambuliaji Gervais Kago kutoka Jamhuri ya Afrika ya Kati rasmi hawatasajiliwa Simbs SC msimu ujao, wakati huo huo wachezaji wanne wazawa mikataba yao inaisha Juni, mwaka huu. Katika mahojiano maalum na BIN ZUBEIRY asubuhi hii, Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’ amewataja wachezaji ambao mikataba yao inaisha ni kipa Ally Mustafa Mtinge ‘Barthez’, mabeki Juma Said Nyosso, Juma Hamisi Jabu na kiungo Uhuru Suleiman Mwambungu ‘Robinho’.
“Hawa wa kigeni kwa kweli hatutawaongezea mikataba, ila hawa wa nyumbani naona wengi wao wakiwa fiti wanacheza vizuri, hasa mashindano ya nyumbani. Tutazungumza nao, tukiafikiana tutawaongezea mikataba,”alisema Kaburu. Kaburu alisema mazungumzo ya mikataba mipya yatafanyika baada ya Simba kumaliza kabisa msimu wa mashindano- ila kama watafuzu kuingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho, zoezi hilo litafanyika Juni. Akimzungumzia mshambuliaji Abdallah Juma wa Ruvu Shooting, ambaye inadaiwa amesajiliwa na klabu hiyo, Kaburu alisema; “Bado”. Akaongeza: “Huyu mchezaji amependekezwa na wajumbe wengi wa Kamati ya Utendaji tumsajili, na yeye ameonyesha nia haswa ya kuchezea Simba, tulichofanya tumezungumza naye tu,”alisema Kaburu, ambaye kesho asubuhi anakwea ‘pipa’ kuelekea Sudan, kuungana na timu yake, ambayo Jumapili itacheza na Al Ahly Shandy katika mchezo wa marudiano wa hatua ya 16 Bora, Kombe la Shirikisho la Afrika.Katika mchezo huo, Simba inahitaji sare tu ili kusonga mbele, kwani mchezo wa kwanza ilishinda mabao 3-0 Dar es Salaam.
STORY BIN ZUBERY
No comments:
Post a Comment