Sunday, May 27, 2012

WAZEE YANGA WAGONGA UKUTA TENA, INABIDI WASUBIRI MKUTANO MKUU ILI WAWEZE KUFANYA MAAMUZI.


 

Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana Mei 26 mwaka huu ili kutoa mwongozo wa nini kifanyike ndani ya Yanga baada ya wajumbe wake kudhaa kujiuzulu. Kamati ya Uchaguzi ya Yanga ilikuwa imeomba mwongozo huo TFF. Baada ya kupata taarifa rasmi kutoka Yanga, Kamati imebaini kuwa Kamati ya Utendaji ya Yanga imekosa akidi baada ya wajumbe wake wengi kujiuzulu hivyo kutokuwa na uwezo wa kufanya uamuzi kwa mujibu wa Ibara ya 32(1) ya Katiba ya klabu hiyo. Hivyo, Kamati imetoa mwongozo kwa Kamati ya Uchaguzi ya TFF ambayo ndiyo msimamizi wa Kamati ya Uchaguzi ya Yanga kuwa ili Kamati ya Utendaji ya Yanga iwe na nguvu za kikatiba kufanya shughuli zake ikiwemo uamuzi wa masuala mbalimbali ndani ya klabu hiyo ni lazima iwe na akidi. Kwa mujibu wa Ibara ya 29(3) ya Katiba ya Yanga nafasi zilizo wazi katika Kamati ya Utendaji zinatakiwa kujazwa katika Mkutano Mkuu wa Kawaida ujao. Pia Kamati imebaini uteuzi wa kujaza nafasi zilizo wazi za wajumbe uliofanywa na Kamati ya Utendaji ya Yanga, Mei 21 mwaka huu ni batili kwa vile Kamati ya Utendaji iliyofanya uteuzi huo haikuwa na akidi. Ili kupata akidi na kufanya uamuzi Kamati ya Utendaji ya Yanga yenye wajumbe 13 inatakiwa kuwa na asilimia 50 ya wajumbe wote, hivyo ili wafanye uamuzi halali hawatakiwi kupungua saba. Kwa wajumbe ambao hawajajiuzulu; Sarah Ramadhan, Mohamed Bhinda, Tito Osoro na Salim Rupia kwa sasa hawawezi kufanya shughuli zozote za Yanga hadi nafasi zilizo wazi katika Kamati ya Utendaji zitakapojazwa. Kama inavyoelekeza Katiba ya Yanga, shughuli za kila siku za klabu hiyo zitaendelea kufanywa na Sekretarieti ya Yanga ambayo kiongozi wake ni Katibu Mkuu.

No comments:

Post a Comment