Thursday, August 9, 2012

JAPAN YAPANIA KUENDELEZA UTEJA KWA MAREKANI KATIKA FAINALI YA SOKA OLIMPIKI.

TIMU ya taifa ya wanawake ya Japan ambao ni mabingwa wa soka wa dunia imepania kuweka rekodi kwa kunyakuwa medali ya dhahabu katika mchezo wa fainali unaotarajiwa kuchezwa baadae leo dhidi ya Marekani. Hiyo pia itakuwa ni nafasi kwa Marekani kulipiza kisasi kwa Japan ambao waliwafunga kwa changamoto ya mikwaju ya penati katika mchezo wa fainali ya Kombe la Dunia mwaka jana baada ya timu hizo kwenda suluhu katika muda wa kawaida. Japan ilitinga katika hatua hiyo baada ya kuisambaratisha Ufaransa katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa Jumatatu wakati Marekani wenyewe waliwasambaratisha majirani zao Canada kwa mabao 4-3 katika mchezo ambao ulichezwa kwa dakika 120 baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 3-3 katika muda wa kawaida. Katika mchezo huo ambao utafanyika katika Uwanja wa Wembley unakadiriwa kuhudhuriwa na mashabiki wapatao 83,000 idadi ambayo itavunja rekodi ya fainali ya olimpiki ya mwaka 1996 kati ya Marekani na China iliyofanyika katika Uwanja wa Sanford jijini Athens, Georgia ambayo ilihudhuriwa na mashabiki 76,489.

No comments:

Post a Comment