Saturday, August 11, 2012

WAMAREKANI WAVUNJA REKODI MBIO ZA VIJITI OLIMPIKI.


TIMU ya Marekani imefanikiwa kuvunja rekodi iliyowekwa miaka 27 iliyopita katika mbio za mita 400 kupokezana vijiti na klushinda medali ya dhahabu katika mashindano hayo ya olimpiki yanayoendelea jijini London. Timu hiyo ambayo ilikuwa na wanariadha Tianna Madison, Allyson Felix, Bianca Knight na Carmelita Jeter walifanikiwa kuvunja rekodi hiyo wakitumia muda wa sekunde 40.82 na kuizidi ile iliyowekwa na wanariadha wa timu ya Ujerumani Mashariki mwaka 1985 ya muda wa sekunde 41.37. Timu ya Jamaica ilishika nafasi ya pili wakiwa nao wamevunja rekodi ya taifa kwa kutumia muda wa sekunde 41.41 huku Ukraine wakishika nafasi ya tatu kwa kutumia sekunde 42.04 na washindi wa nne kuwa Nigeria. Marekani walishindwa kufuzu katika fainali ya mbio hizo katika michuano ya olimpiki iliyofanyika jijini Beijing mwaka 2008 lakini baada ya kufanikiwa kutinga fainali katika mbio za mwaka huu wakiwa wanaongoza hawakurudi nyuma mpaka waliponyakuwa medali hiyo ya dhahabu. Mbio hizo za kupokezana vijiti zitaendelea tena leo kwa upande wa wanaume ambao timu ya Jamaica ambayo inaongozwa na Usain Bolt na Yohane Blake ikipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment