Sunday, September 16, 2012

PUYOL NJE WIKI SITA.

NAHODHA wa klabu ya Barcelona ya Hispania, Carles Puyol anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki sita baada ya kuanguka vibaya na kuumia goti wakati timu yake ilipoibuka na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Getafe jana. Puyol mwenye umri wa miaka 34 alijaribu kuendelea na mchezo baada ya kupatiwa matibabu kufuatia tukio hilo lakini hakuweza kucheza sana baada ya kutolewa dakika ya 57 na nafasi yake kuchukuliwa na Javier Mascherano. Kocha wa Barcelona Tito Vilanova amesema kuwa Puyol amekuwa mchezaji muhimu kwa kikosi hicho hivyo wanaamini atapona mapema ili aweze kuendelea na majukumu yake. Puyol amerejea uwanjani hivi karibuni baada ya kuumia katika mchezo dhidi ya Osasuna mwezi uliopita na pia alifanyiwa upasuaji katika mguu wake wa kulia Mei mwaka huu na kulazimika kukosa michuano ya Ulaya ambapo Hispania waliibuka mabingwa. Kama vipimo atakavyochuliwa mchezaji huyo vikithibitisha kwamba atakosa kuwa dimbani kwa muda huo, inamaanisha Puyol atakosa mchezo wa ufunguzi wa ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Spartak Moscow utakaochezwa Jumatano pamoja na mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya mahasimu wao Real Madrid Octoba 7 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment