Monday, September 24, 2012

VETTEL ANUSANUSA TAJI LA DUNIA LA LANGALANGA.

Dereva nyota wa mashindano ya langalanga Sebastian Vettel ameonyesha kurejesha makali yake na kurejesha matumaini ya kunyakuwa taji la michuano hiyo kwa mwaka huu baada ya kushinda michuano ya Grand Prix ya Singapore. Ushindi huo unamsogeza karibu na kiongozi wa mbio hizo Fernando Alonso ambaye ana alama 29 zaidi ya Vettel huku yakiwa yamebakia mashindano sita pekee kwa msimu huu. Wadau wengi wa mbio hizo wamesema Vettel ambaye yuko katika timu ya Red Bull ana nafasi kubwa ya kunyakuwa taji lake la tatu la Dunia msimu huu baada ya dereva wa MacLaren Lewis Hamilton kushindwa kutamba katika mbio za Singapore baada ya gari lake kuharibika. Vettel ambaye pia atashiriki mbio za Grand Prix za Japan wiki ijayo amesema ameridhika na nafasi aliyopo hivi sasa baada ya kushinda mashindano ya Singapore na ni matarajio yake ataendelea kufanya vizuri huko mbele ingawa amedai bado ana upinzani mkubwa. Msimamo wa madereva hao katika orodha na alama walizonazo ni Alonso alama 194, Vettel alama 169, Kimi Raikkonen alama 149, Hamilton alama 142 na Mark Webber mwenye alama 132.

No comments:

Post a Comment