Thursday, October 25, 2012

MADRID, MILAN, CITY, ARSENAL ZAANGUKIA PUA CHAMPIONS LEAGUE.

KLABU za Real Madrid, Manchester City, Arsenal na AC Milan zimeshindwa kutamba katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kukubali vipigo katika michezo yao ya jana na kujiweka katika nafasi ngumu ya kusonga mbele katika michuano hiyo. Timu za Ujerumani zilionyesha kiwango bora jana baada ya mabingwa wa Bundesliga Borussia Dortmund kuwafunga mabingwa mara tisa wa michuano hiyo Madrid kwa mabao 2-1 nyumbani wakati mahasimu wao Schalke 04 wenyewe walifanikiwa kupata ushindi ugenini kwa kuingamiza Arsenal kwa mabao 2-0. Mabingwa mara saba wa michuano hiyo Milan wameendelea kucheza kwa kiwango cha chini baada ya kukubali kipigo cha bao 1-0 nyumbani kwa Malaga timu ambayo imekuwa ikisumbuliwa na ukata lakini wamekuwa wakifanya vyema katika kundi C wakiwa na alama nyingi zaidi. Mabingwa wa Ligi Kuu chini Uingereza, Manchester City ambao waliishia katika hatua ya makundi msimu uliopita nao wamejikuta wakijiweka tena katika nafasi ya hatari ya kutoka baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka Ajax Amsterdam na kujikuta wakishika mkia katika kundi D kwa kukusanya alama moja katika michezo mitatu.

No comments:

Post a Comment