Tuesday, October 23, 2012

PIQUE KUIKOSA CELTIC.

MENEJA wa klabu ya Barcelona, Tito Vilanova amesema kuwa beki wake wa kati Gerard Pique atakosa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Celtic leo usiku baada ya kushindwa kupona mguu. Majeruhi katika kikosi cha Vilanova limekuwa tatizo sugu hususani mabeki wake tegemeo kama Eric Abidal, Carles Puyol na Dani Alves kupata majeruhi ya mara kwa mara kitu ambacho kimekuwa kikiwapa wakati mgumu msimu huu. Mwishoni mwa wiki Barcelona ilipata ushindi wa tabu wa mabao 5-4 dhidi ya Deportivo Coruna huku ikishuhudia beki wake wa kati aliyebakia Sergio Busquets naye akipewa kadi nyekundu katika mchezo huo. Lakini Vilanova amesema kuwa kuwakosa nyota wake hao haiwezi kuwa sababu ya wao kushindwa kufanya vyema katika mchezo wa leo. Barcelona ndio wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu nchini Hispania maarufu kama La Liga wakifuatiwa na Atletico Madrid ambao wamepisha kwa tofauti ya mabao lakini wakiwa wameruhusu wavu wao kutikiswa mara 11 sawa na Osasuna ambao wanashika mkia katika ligi hiyo.

No comments:

Post a Comment