Wednesday, October 17, 2012

SJIUZULU NG'O - SENGHOR.

RAIS wa Shirikisho la Soka nchini Senegal-FSF, Augustin Senghor ametangaza kuwa kamati yake ya utendaji haitajiuzulu pamoja na wadau wengi wa soka nchini humo kuwataka kufanya hivyo kufuatia timu ya taifa ya nchi hiyo kushindwa kufuzu michuano ya Mataifa ya Afrika mwakani. Senghor alijibu mashambulizi ya wapinzani wake na kuwaita wahujumu wa maendeleo ya soka la nchi hiyo na kutangaza kuwa FSF imetoa malalamiko dhidi ya mtu asiyejulikana aliyechangia kuvurugika kwa mchezo wao dhidi ya Ivory Coast katika dakika ya 76. Rais huyo aliendelea kutamba kuwa wamechaguliwa kushikilia wadhifa huo kwa kipindi cha miaka minne hivyo hawawezi kujiuzulu kwa ajili ya tukio la vurugu lililotokea Jumamosi na wale wanaotaka wajiuzulu wanapoteza muda wao. Nahodha wa zamani wa timu ya taifa ya nchi hiyo El Hadji Diouf alimwambia rais wa FSF na kamati yake ya utendaji kuwa wanatakiwa kujiuzulu na kumtaja mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Olympique Marseille Pape Diouf kuchukua nafasi hiyo ili kusuka upya mfumo wa soka nchini humo. Mapema Jumatatu FSF ilimtuhumu ingawa sio moja kwa moja Diouf kulipia tiketi zaidi ya 1,000 na kuzigawa kwa wahuni ili wavuruge mchezo wa Jumamosi iliyopita shutuma ambazo zilipingwa vikali na nyota huyo.

No comments:

Post a Comment