Tuesday, October 9, 2012

SUDAN YANYANG'ANYWA ALAMA NA FIFA.

Shirikisho la Soka la Dunia-FIFA limeinyang’anya ushindi wa mabao 2-0 Sudani iliyopata dhidi ya Zambia katika mchezo wa kufuzu michuano ya Kombe la Dunia 2014 kwasababu mmoja wa wachezaji aliyefunga mabao hayo hakuruhusiwa kucheza. Kamati ya nidhamu ya FIFA ilifafanua katika taarifa yake kuwa mchezaji huyo aitwaye SAIF ALI hakuruhusiwa kucheza katika mchezo huo uliochezwa June 2 mwaka huu jijini Khartoum. Zambia walilalamika kuwa ALI alicheza katika mchezo huo pamoja na kuwa na kadi mbili za njano katika michezo miwili tofauti ukiwemo mchezo ambao Zambia iliifunga Sudan katika mchezo wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika uliochezwa Februari mwaka huu. FIFA ilikubaliana na malalamiko hayo ya Zambia baada ya kufanya uchunguzi na kuipa ushindi wa mabao 3-0 na pointi tatu nchi hiyo huku ikilitoza faini Shirikisho la Soka la Sudan ya dola 6,430. Zambia sasa inaongoza katika kundi D ikiwa na alama sita katika michezo miwili waliyocheza na Sudan imedondoka mpaka nafasi ya tatu ikiwa na alama moja, Ghana wako nafasi ya pili wakiwa na alama tatu na Lesotho ni ya mwisho wakiwa na alama moja.

No comments:

Post a Comment