Monday, October 22, 2012

UEFA YAMBANA TERRY.

BEKI wa klabu ya Chelsea ataamriwa na Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kuvaa kitambaa mkononi chenye maandishi ya kupinga ubaguzi wa rangi michezoni kama atapewa unahodha wa klabu hiyo wakati wa mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Shakhtar Donetsk kesho usiku. Hatua hiyo imekuja ikiwa ni wiki moja imepita toka nyota huyo alipoadhibiwa na Chama cha Soka nchini Uingereza-FA kwa kumfanyia vitendo vya kibaguzi beki wa Queens Park Rangers Anton Ferdinand. Katika michuano hiyo ya ligi ya mabingwa ambayo itachezwa leo na kesho manahodha wa vilabu vyote vinavyoshiriki michuano hiyo watatakiwa kuvaa vitambaa vyenye maandishi hayo ikiwa ni kuadhimisha wiki ya kupiga vita vitendo hivyo michezoni. Wiki iliyopita Terry alikubali adhabu ya kufungiwa michezo minne na kutozwa faini ya paundi 220,000 adhabu ambayo atakuwa akiitumikia katika michezo ya mashindano ya nyumbani pekee. Katika taarifa iliyotolewa na UEFA timu zote zitakazocheza michuano hiyo wiki hii zitasindikizwa na watoto ambao watakuwa wamevalia fulana zenye maandishi ya kupiga vita ubaguzi huku manahodha wakiwa wamevaa maandishi hayo katika vitambaa mikononi mwao.

No comments:

Post a Comment