WANADADA nyota wa mchezo wa tenisi, Serena Williams na Maria Sharapova wanatarajiwa kukutana katika mchezo wa fainali ya michuano ya WTA jijini Istanbul baadae leo. Williams kutoka Marekani ambaye anashika namba tatu katika orodha za ubora duniani kwa upande wanawake alifanikiwa kutinga fainali baada ya kumfunga Agnieska Radwanska kwa 6-2 6-1 akitumia muda wa dakika 61. Sharapova ambaye anashika namba mbili alifanikiwa kutinga hatua hiyo baada ya kumfunga mwanadada namba moja katika orodha hizo Victoria Azarenka kwa 6-4 6-2. Azarenka ambaye alijihakikishia nafasi ya kumaliza mwaka akiwa katika namba moja baada ya kumfunga Li Na wa China katika mchezo huo alionekana kupata majeraha katika mguu wake kulia hivyo kushindwa kuhimili vishindo vya mpinzani wake. Sharapova bingwa wa michuano ya wazi ya Ufaransa leo aaingia uwanjani akitafuta taji lake la pili la michuano hiyo ambayo mara ya mwisho alinyakuwa mwaka 2004 lakini atakumbana na wakati mgumu kwa Williams ambaye ameshinda taji hilo mara sita na sasa yuko katika kiwango cha juu kabisa.
No comments:
Post a Comment