KOCHA wa timu ya taifa ya Uganda, Bobby Williamson ameonyesha kutofurahishwa na baadhi ya sheria za Shirikisho la Soka barani Afrika-CAF baada ya kikosi kushindwa kufuzu katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika ambayo itafanyika nchini Afrika Kusini 2013. Williamson alishindwa kuelewa kwa nini sare waliyopata iamuliwe kwa changamoto ya mikwaju ya penati baada ya Uganda kusawazisha bao ambalo walifungwa na Zambia katika mchezo wa kwanza timu hizo zilipokutana. Akihojiwa mara baada ya mchezo huo Williamson amesema kuwa mchezo ulipaswa uchezwe katika muda wa nyongeza badala ya kwenda moja kwa moja katika matuta ambayo Zambia walishika kwa 9-8. Hata hivyo Williamson alisifu kiwango kilichoonyeshwa na kikosi chake kwenye mchezo huo huku akimponda golikipa wa Zambia Kennedy Mweene kwa kupoteza katika dakika za mwisho za mchezo huo. Matokeo hayo yanamaanisha Uganda inabidi iendelee kusubiri miaka mingine miwili zaidi ili iweze kujaribu tena kufuzu michuano hiyo ambayo amara ya mwisho walicheza miaka 34 iliyopita.
No comments:
Post a Comment