Saturday, November 17, 2012

ABO TRIKA KUTUNDIKA DARUGA BAADA YA CHAMPIONS LEAGUE.

KOCHA wa zamani wa timu ya Taifa ya Misri, Hassan Shehata ameweka wazi kuwa nahodha wa timu ya Al Ahly Mohammed Abo Trika atastaafu rasmi kucheza soka baada ya fainali za michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika. Shehata ambaye kwasasa anafundisha katika klabu ya Al Arabi ya Qatar amesema kuwa alizungumza na Trika aliyemuomba ushauri kuhusiana na uamuzi wake wa kustaafu. Kocha huyo ambaye alianza kufanya kazi na Trika wakati alipopewa mikoba ya kuinoa timu ya taifa ya Misri aliendelea kusema kuwa pamoja na kujaribu kumshawishi nyota huyo aachane na maamuzi ya kustaafu ilishindikana. Shehata amesema anaamini mchezaji bado ana uwezo wa kucheza miaka mingine miwili au mitatu kabla ya kustaafu lakini anadhani hilo halitawezekana kutokana na mchezaji huyo kutotaka kubadilisha msimamo wake. Shehata ambaye anajulikana kama Godfather aliomba bodi ya Al Ahly kujaribu kumshawishi nyota huyo mwenye umri wa miaka 34 ili abakie kwa miaka mingine kadhaa katika ulimwengu wa soka.

No comments:

Post a Comment