Thursday, November 1, 2012
BIN HAMMAM AGONGA UKUTA CAS.
MGOMBEA wa zamani wa urais wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA Mohamed bin Hammam ameshindwa rufani yake ya kutengua adhabu ya siku 90 alizopewa wakati uchunguzi wa suala la rushwa dhidi yake ukiendelea. Bin Hammam ambaye ni raia wa Qatar alikata rufani kuhusu kufungiwa kwake huko akidai lilikuwa ni suala la kisiasa baada ya kujitokeza kugombea nafasi hiyo na Sepp Blatter Mei mwaka jana. Bin Hammam ambaye pia amewahi kuwa rais wa Shirikisho la Soka barani Asia-AFC alishinda rufani yake ya kufungiwa maisha kwasababu ya kukutwa na hatia ya kuhonga wapiga kura Julai mwaka huu lakini FIFA ilianza uchunguzi mpya dhidi yake juu matumizi mabaya ya fedha wakati akiwa rais wa AFC. Baada ya kushindwa kuishawishi kamati ya rufani ya FIFA kutengua adhabu ya kufungiwa siku 90 Bin Hammam aliamua kupeleka shauri hilo katika Mahakama ya Usuluhishi ya Michezo-CAS ambako nako maegonga mwamba. Kamati ya maadili ya FIFA ikiongozwa na wakili wa zamani wa Marekani Michael Garcia wataendelea na uchunguzi juu matumizi mabaya ya fedha aliyofanya Bin Hammam kipindi hicho akiwa rais wa AFC.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment