Wednesday, November 7, 2012

PORTO, MALAGA ZAGONGA HODI 16 BORA CHAMPIONS LEAGUE.

MABINGWA wa zamani wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Porto ya Ureno na Malaga ya Hispania zimekuwa timu za kwanza kutinga katika hatua ya pili ya michuano hiyo huku zikiwa na michezo miwili mkononi baada ya kufanya vyema katika michezo yao ya jana usiku. Porto ambao ni mabingwa wa michuano hiyo mwaka 1987 na 2004 ndio wanaongoza kundi A wakiwa na alama 10 baada ya kufanikiwa kutoa sare ya bila ya kufungana na Dynamo Kiev na kujihakikishia nafasi ya kuingia hatua ya 16 bora. Malaga ambayo inamilikiwa na tajiri kutoka Qatar nayo kwa mara ya kwanza imefanikiwa kutinga mzunguko wa pili baada ya kutoa sare ya bao 1-1 na Ac Milan ya Italia na kuongoza kwa alama 10 kwenye kundi C. Katika michezo mingine iliyochezwa jana Borussia Dortmund ilibaki kidogo nao wakate tiketi ya kusonga mbele katika kundi D kabla ya bao la kusawazisha la mshambuliaji nyota wa Real Madrid Mesut Ozil kupelekea timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2. Dortmund wanaoongoza kundi hilo wakiwa na alama nane na Madrid wenye alama saba ndizo timu zinazopewa nafasi ya kusonga mbele baada ya Manchester City kushindwa kuifunga Ajax Amsterdam na kutoka sare ya mabao 2-2 hivyo kupelekea mabingwa hao wa Uingereza kujiweka katika mazingira ya kushindwa kufuzu michuano hiyo kwa mara ya pili mfulilizo. Katika kundi B nako Arsenal walishindwa kulinda ushindi wao wa mabao 2-0 waliopata mapema katika kipindi cha kwanza dhidi ya Schalke O4 ya Ujerumani na kujikuta wakitoka sare ya mabao 2-2 na kubakia nyuma ya wajerumani hao kwa lama moja.

No comments:

Post a Comment