Thursday, November 8, 2012
WACHEZAJI WATANO WAFUNGIWA NCHINI UFARANSA.
KIKUNDI cha wachezaji wa kimataifa wa Ufaransa chini ya miaka 21 wamefungiwa kushiriki michezo ya kimataifa kwasababu ya kutoroka kambini wakati wa mchezo wa kufuzu michuano ya Ulaya mwezi uliopita. Wachezaji waliopata adhabu hiyo ni pamoja na Yann Mvila na Chris Mavinga wanaocheza katika klabu ya Rennes, Wissam Ben Yedder anayecheza timu ya Toulouse, Antoine Griezmann wa Real Sociedad na Mbaye Niang anayekipiga AC Milan. Wachezaji wote hao wamefungiwa kucheza michezo ya kimataifa mpaka Desemba 31 mwakani kasoro Mvila ambaye amepata adhabu kubwa zaidi ya kufungiwa mpaka Juni 30 mwaka 2014 adhabu ambayo imetolewa na Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka nchini Ufaransa. Wachezaji hao walitoroka katika kambi yao iliyopo katika mji uliopo Kaskazini mwa mji wa Le Havre na kwenda jijini Paris kujirusha na kupelekea timu yao kufungwa na Norway bao 1-0. Mvila amekuwa akioywa na FFF mara kwa mara kwa kukataa kushikana mikono na aliyekuwa na kocha wa timu ya taifa ya nchi hiyo Laurent Blanc wakati alipotolewa wakati wa robo fainali ya michuano ya Ulaya iliyofanyika mwaka huu katika mchezo baina ya timu hiyo na Hispania.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment