Wednesday, December 26, 2012

AFCON 2013: ZAMBIA, ANGOLA ZAWA TIMU ZA KWANZA KUWASILI AFRIKA KUSINI.

Timu za taifa za Angola na mabingwa wa Afrika Zambia zimekuwa za kwanza kuwasili nchini Afrika Kusini kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika ambapo zimebaki wiki tatu kabla ya kuanza. Timu zote mbili zimefikia jijini Johannesburg na zitabakia hapo katika kipindi chote watakachokuwa wakifanya maandalizi yao kabla ya kuanza michuano hiyo Januari 19, 2013. Angola imesafiri na wachezaji wake wote 20 ambao wanacheza katika ligi ya nyumbani huku waliopo Ulaya wakitegemewa kuungana na wenzao wiki mbili kabla ya michuano hiyo. Shirikisho la Soka nchini Angola limedai kuwa wakiwa nchini humo wanatarajia kucheza michezo kadhaa ya kirafiki dhidi ya timu za Msumbiji, Tanzania na Zambia wakiwa hapohapo jijini Johannesburg lakini bado wako katika mazungumzo juu ya tarehe za kuchezwa mechi hizo. Algeria na Morocco zinatarajiwa kuwa timu zitakazofuata kuwasili nchini humo kwa ajili ya michuano hiyo siku baada ya kuanza mwaka mpya.

No comments:

Post a Comment