Wednesday, December 5, 2012

WACHEZAJI WA ERITREA WALIOTOWEKA WAJITOKEZA NA KUOMBA HIFADHI YA UKIMBIZI.

WACHEZAJI 17 na kiongozi mmoja wa timu ya taifa ya Eritrea waliokuwa wametoweka katika hoteli yao jijini Kampala, Uganda Jumapili wamonekana. Wachezaji hao walikutana na Waziri wan chi hiyo anayeshughulika masuala ya maafa, Musa Echweru na kuomba hifadhi kama wakimbizi huku wenzao wengine waliobakia ambao ni wachezaji wawili na viongozi watano wakirejea nyumbani Jumanne. Echweru alithibitisha kuwasiliana na wachezaji hao na kusema kuwa wamepeleka suala suala hilo kwa mamlaka husika ili waweze kulishughulikia. Eritrea walitolewa katika mashindano ya Kombe la Cecafa Jumamosi iliyopita na timu nzima ilitakiwa kurejea nyumbani Jumanne. Hiyo imekuwa ni tabia ya kawaida kwa wachezaji wa Eritrea kutoweka mara baada ya mechi za mashindano ambapo mwaka 2007 katika michuano hiyo iliyofanyika nchini Tanzania wachezaji 12 walipotea kabla ya kurudia tukio kama hilo miaka miwili baadae katika mashindano kama hayo yaliyofanyika nchini Kenya. Matukio ya uvunjaji wa sheria za haki za binadamu na kukosekana kwa uhuru wa vyombo vya habari pamoja na uhuru wa kisiasa nchini Eritrea ndio inachangia kwa kiasi kikubwa wachezaji hao kuamua kutoweka na kushindwa kurudi kwao huku wakiomba hifadhi ya kikimbizi katika nchi walizokwenda.

No comments:

Post a Comment