Sunday, January 27, 2013

AFCON 2013: ALGERIA YAFUNGISHWA VIRAGO MAPEMA, IVORY COAST SAFI.

ALGERIA imekuwa timu ya kwanza kuyaaga mashindano ya Mataifa ya Afrika-Afcon baada ya kukubali kipigo cha pili mfululizo kutoka kwa Togo katika mchezo wa kundi D uliochezwa katika Uwanja wa Royal Bafokeng nchini Afrika Kusini. Algeria ambayo inashika nafasi ya 22 katika orodha za ubora duniani ilikubali kipigo cha mabao 2-0 na kuwa timu ya kwanza kigogo kuyaaga mashindano hayo katika hatua ya makundi baada ya kufungwa pia katika mchezo wa kwanza dhidi Tunisia. Katika michezo mingine iliyochezwa jana ya kundi hilo Ivory Coast walifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kuifunga Tunisia kwa mabao 3-0 yaliyofungwa na Gervinho, Yaya Toure na Didier Ya Konan. Ivory Coast ambayo inapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo inakuwa timu ya kwanza kusonga mbele katika kundi hilo baada ya kujikusanyia alama zote sita katika michezo miwili waliyocheza. Mzunguko wa mwisho katika kundi hilo utazikutanisha timu za Ivory Coast na Algeria ambao tayari wameshayaaga mashindano hayo huku mchezo mgumu ukitarajiwa kuwa kati ya Tunisia na Togo ambao wote watakuwa wakitafuta nafasi ya kusonga mbele.

No comments:

Post a Comment