Monday, January 28, 2013

AFCON 2013 YAFIKIA PATAMU.

MICHUANO ya Mataifa ya Afrika-Afcon inatarajiwa kuendelea tena baadae leo ambapo timu nne kundi B zitakuwa zikitafuta nafasi ya kusonga mbele katika michezo yao ya mwisho. Katika michezo ya leo Ghana ambao wanapewa nafasi kubwa ya kusonga mbele kama vinara wa kundi hilo watachuana na Niger ambayo nayo inaweza kupata nafasi kama wakifanikiwa kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo-DRC timu ambayo imekuwa ikionyesha kandanda la kuvutia katika michuano hiyo inatarajiwa kusaka ushindi wa kwanza dhidi ya timu ngumu ya Mali baada ya kutoka sare katika michezo yake miwili iliyopita. Katika michezo ya kundi A iliyochezwa jana, timu ngeni katika michuano hiyo Cape Verde iliandika historia nyingine kwa kuilaza Angola kwa mabao 2-1 na kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo. Cape Verde nchi ambayo ni kisiwa kinachokadiriwa kuwa na watu wapatao 500,000 inajiunga na wenyeji Afrika Kusini ambao nao walisonga mbele wakiwa vinara wa kundi lao pamoja na Ivory Coast ambao walitinga hatua hiyo mapema.

No comments:

Post a Comment