Sunday, January 13, 2013

AYEW AREJEA KATIKA KIKOSI CHA MARSEILLE BAADA YA KUPONA.

WINGA machachari wa kimataifa wa Ghana na klabu ya Olympique Marseille ya Ufaransa, Andre Ayew ambaye aliondolewa katika kikosi cha timu ya taifa ya nchi hiyo, ameitwa katika kikosi cha Marseille ambacho kinatarajia kucheza na Sochaux katika mchezo wa Ligi Kuu nchini Ufaransa. Taarifa iliyolewa na mtandao wa klabu hiyo imedai kuwa Ayew ambaye ameichezea Ghana mechi 44 amepona majeraha ya paja aliyopata wakati wa mazoezi na klabu yake siku 10 zilizopita. Ayew mwenye umri wa miaka 23 ambaye ni mtoto wa nguli wa zamani wa Ghana Abeid Pele, alitarajiwa kujiunga na kikosi cha timu ya taifa mwishoni mwa wiki iliyopita kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya majeraha yake lakini hakutokea kwa wakati kitendo ambacho kilipelekea kocha Kwesi Appiah kumuengua kwa ajili ya michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon. Kama ilivyo kwa Ayew, golikipa wa Togo Kossi Agassa naye pia anatarajia kuwepo katika kikosi cha Marseille Jumapili pamoja na kuenguliwa katika michuano ya Afcon kutokana na kupata majeraha ya mguu. Michuano ya Afcon inatarajiwa kuanza kutimua vumbi Januri 19 na kumalizika Februari 10 mwaka huu.

No comments:

Post a Comment