Wednesday, January 23, 2013

CAF YAITOZA FAINI ETHIOPIA KUFUATIA VURUGU ZA MASHABIKI WAKE.

SHIRIKISHO la Soka barani Afrika-CAF limelitoza faini ya dola 10,000 Shirikisho la Soka la Ethiopia baada ya mashabiki wake kutupa mavuvuzela pamoja na chupa za maji uwanjani wakati wa mchezo wao dhidi ya Zambia ambao walitoka sare ya bao 1-1 Jumatatu. CAF ilitangaza kuwa nusu ya adhabu hiyo ya dola 10,000 itasamehewa kama tu mashabiki wa Ethiopia hawatarudia tukio hilo katika kipindi chote cha mashindano. Ethiopia inayoshiriki michuano ya Mataifa ya Afrika-Afcon kwa mara ya kwanza baada ya miaka 31 ina mashabiki wengi waliokuja kuiunga mkono timu yao lakini mchezo wao wa kwanza uliochezwa katika Uwanja wa Mbombela uliingia dosari baada ya mwamuzi Eric Otogo-Castane alipompa kadi nyekundu golikipa Jemal Tassew muda mchache kabla ya mapumziko. Mara baada ya mwamuzi huyo kutoa kadi vuvuzela na chupa za maji zilimiminika uwanjani zikitokea jukwaani huku makocha na wachezaji wa akiba wakijificha wasiumizwe na vitu hivyo wakati mtangazaji uwanjani hapo alikiwaomba mashabiki hao kutulia. Mashabiki hao wa Ethiopia pia wanaweza kufungiwa kuingia uwanjani katika mchezo wa Ijumaa dhidi ya Burkina Faso labda CAF ipate uhakika kutoka EFF kuwa watawadhibiti mashabiki wao.

No comments:

Post a Comment