Tuesday, January 29, 2013

USALAMA NI JAMBO LINALOPEWA KIPAUMBELE - VALCKE.

MAOFISA wa ngazi za juu wa michezo wamesisitiza kuwa usalama litakuwa jambo linalopewa kipaumbele nchini Brazil katika michuano ya Kombe ya Dunia na Olimpiki ikiwa ni tahadhari kufuatia moto uliozuka katika klabu moja ya usiku na kuua watu wapatao 231. Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Jerome Valcke amesema kuwa ajali iliyotokea huko Santa Maria mji uliopo kusini mwa nchi hiyo ni mojawapo ya ajali mbaya zaidi kuwahi kutokea. Hatahivyo Valcke amesema ajali hiyo ya moto haihusiani na usalama ndani ya viwanj ambavyo vitatumika kwa ajili ya michuano ya Kombe la Shirikisho inayotarajiwa kuanza kutimua vumbi June 15 hadi 30 mwaka huu pamoja na ile ya Kombe la Dunia mwakani. Amesema katika michuano hiyo wameandaa watu na kuwapa mafunzo ya kutosha na kuwa na uwezo kuwaondoa watu waliojaa uwanjani katika muda wa dakika nane pindi tukio la hatari linapotokea. Naye mkurugenzi wa mawasiliano wa kamati ya maandalizi ya michuano ya Olimpiki 2016, Carlos Vilanova amesema tukio la moto lililotokea linaweza kutokea mahala popote duniani na wala halihusiani na uwezo wa Brazil kuandaa mashindano makubwa. Vilanova amesema nchi hiyo imekuwa ikiandaa matamasha makubwa kwa miaka mingi kama Rio Carnaval na mafataki yanayorushwa katika kipindi cha mwaka mpya kwenye ufukwe wa Copacabana ambao hukusanya watu zaidi ya milioni mbili lakini hakujawahi kutokea tukio lolote baya.

No comments:

Post a Comment