Thursday, March 14, 2013
BLATTER APONDA MPANGO WA UEFA KUANDAA EURO 2020 KATIKA NCHI 13.
RAIS wa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA, Sepp Blatter amekosoa wazo la Shirikisho la Soka barani Ulaya-UEFA kufanya michuano ya bara hilo katika baadhi ya nchi. Kauli hiyo ya Blatter imekuja kufuatia UEFA kupanga kuandaa michuano ya Ulaya 2020 katika nchi 13 tofauti katika bara hilo badala ya nchi moja kama ilivyo hivi sasa. Michuano ya Ulaya 2020 itafanyika katika nchi mbalimbali barani Ulaya ikiwa kama sehemu ya kutimiza miaka 60 toka kuanzishwa kwa michuano hiyo uamuzi ambao umekuwa ukipingwa na wadau mbalimbali katika miezi ya hivi karibuni. Blatter amesema alishamwambia rais wa UEFA Michel Platini kuwa kiongozi wa zamani wa Libya hayati Mouamar Gaddafi alishampatia mpango kama huo wakati akitafuta nchi yake iwe mwenyeji wa michuano ya Kombe la Dunia mwaka 2010 lakini alimkatalia. Hivyo mpango wa Platini sio mpya. Blatter aliendelea kudai kuwa michuano hiyo inatakiwa kuchezwa katika moja ili kutengeneza utambulisho na msisimko kama ilivyokuwa michuano ya Kombe la Dunia iliyofanyika nchini Ujerumani mwaka 2006. Miji itakayopewa dhamana ya kuandaa michuano ya Ulaya 2020 inatarajiwa na UEFA kutangazwa Septemba 2014.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment