Monday, March 25, 2013

COSTA RICA WAKATA RUFANI.

SHIRIKISHO la Soka nchini Costa Rica limekata rufani rasmi kuutaka mchezo wao dhidi ya Marekani ambao walifungwa kwa bao 1-0 urudiwe kutokana na hali mbaya ya hewa iliyoathiri mchezo huo. Bao lililofungwa na Clint Dempsey katika dakika ya 16 ndio bao pekee katika mchezo huo ambao mara kwa mara ulikuwa ukisimamishwa ili kupisha wafanyakazi kutoa barafu nyingi ambazo zilikuwa zikianguka uwanjani. Katika taarifa yao rais wa shirikisho hilo Ronaldo Villalobos amedai kuwa picha za mnato na video vimetumwa Shirikisho la Soka Duniani-FIFA ili kuipa nguvu rufani yao na kuwataka waamuzi waliochezesha mchezo huo kuchukuliwa hatua za kisheria. Pia katika taarifa hiyo Villalobos amedai kuwa katika sheria za soka wafanyakazi hawaruhusiwi kuingia uwanjani wakati wa mchezo ili kusafisha wakati akidai pia ilikuwa kazi kubwa mpira kuchezwa kutokana na barafi nyingi iliyokuwepo. Kocha wa Costa Rica Jorge Luis Pinto alitaka mchezo huo usogezwe mbele lakini kocha wa Marekani Jurgen Klinsmann alisisitiza kuwa ni sawa mchezo huo kuendelea kwakuwa wachezaji wa pande zote mbili wanakumbana na hali hiyo. Matokeo hayo ya Ijumaa yanaifanya Costa Rica kushika mkia katika kundi lao wakiwa na alama moja katika mechi mbili walizocheza huku Marekani wakiwa katika nafasi ya pili kwa kupata alama tatu.

No comments:

Post a Comment