Saturday, March 23, 2013
HISPANIA YANG'ANG'ANIWA ULAYA.
Mabingwa wa Dunia na Ulaya, Hispania jana walishindwa kutamba baada ya kung’ang’aniwa sare na Finland lakini Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Uholanzi zilifanikiwa kupata ushindi wakati mataifa makubwa yalipokuwa yakitafuta tiketi ya kucheza michuano ya Kombe la Dunia 2014 jana. Hispania ambao waling’ang’aniwa sare ya bao 1-1 na Finland katika mchezo uliochezwa huko jijini Gijon wamepoteza nafasi yao ya kwanza waliyokuwa wakishikilia katika kundi I ambapo sasa Ufaransa ndio wanaongoza kundi hilo baada ya kufanikiwa kuigaragaza Georgia kwa mabao 3-1. Katika michezo mingine Uingereza ilipata ushindi mnono kwa kuichakaza San Marino mabao 8-0 na vigogo wengine Ujerumani wao walipata ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Kazakhstan wakai Uholanzi wao waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Estonia mabao ambayo yote yalifungwa katika kipindi cha pili. Ubelgiji wao waliendelea kujisogeza katika kupata nafasi ya kwenda nchini Brazil 2014 baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Macedonia na kukaa kileleni katika kundi A wakiwa alama sawa na Croatia ambao nao walifanikiwa kuwatandika mahasimu wao Serbia kwa mabao 2-0. Mechi zingine ni Bosnia ilifanikiwa kuifunga Ugiriki kwa mabao 3-1, Ureno walishindwa kutamba mbele ya Israel kwa kung’ang’aniwa sare ya mabao 3-3 na Sweden nao walishindwa kuitambia Ireland kwa kutoka nayo sare ya bila kufungana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment