MSHAMBULIAJI nguli wa zamani wa Uruguay, Luis Cubilla ambaye amecheza Kombe la Dunia mara tatu akiwa na timu ya taifa ya nchi hiyo na akiwa kocha ameshinda mara mbili Kombe la Libertadores akiwa na klabu ya Olimpia ya Paraguay, amefariki dunia akiwa na miaka 72. Chama cha soka nchini Uruguay-AUF kilithibitisha taarifa hizo katika mtandao wake kwamba Cubilla mmoja wa wachezaji waliopata mafanikio zaidi nchini humo amefariki duniani kwa ugonjwa wa kansa ya utumbo katika mji mkuu wa Paraguay, Asuncion alipokuwa akiishi. Akiwa mchezaji, Cubilla alikuwa sehemu ya kikosi cha Uruguay ambacho kilishiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka 1962, 1970 na 1974 ambao mwaka 1970 nchi hiyo ilitinga nusu fainali ya michuano hiyo kabla ya kupoteza kwa Brazil kwa kufungwa mabao 3-1. Nguli huyo amecheza misimu miwili katika klabu ya Barcelona ya Hispania na kushinda Kombe la Mfalme kabla ya kutimkia Argentina katika klabu ya River Plate.
No comments:
Post a Comment