MWANADADA nyota katika tenisi Maria Sharapova amefanikiwa kutinga fainali ya michuano ya wazi ya Sony ambapo sasa atachuana na Serena Williams. Williams ambaye anashika namba moja katika orodha za ubora duniani alihitaji dakika 65 kumfunga bingwa mtetezi wa michuano hiyo Agnieska Radwanska kwa 6-0 6-3 wakai Sharapova alimgaragaza Jelena Jankovic kwa 6-2 6-1. Pamoja na kiwango kizuri alichonacho Sharapova ambaye ni raia wa Urusi, Williams ndio anapewa nafasi kubwa ya kunyakuwa taji hilo ambapo katika mechi 12 walizokutana Williams ameshinda 10. Kwa upande wa wanaume bingwa wa michuano ya US Open na olimpiki Andy Murray amefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kumfunga Marin Cilic wa Croatia kwa 6-4 6-3. Murray raia wa Uingereza ambaye anashika namba mbili katika orodha za ubora duniani kwa upande wa wanaume anatarajiwa kuchuana na Richard Gasquet wa Ufaransa katika kutafuta nafasi ya kucheza fainali ya michuano hiyo Jumapili.
No comments:
Post a Comment