Thursday, March 21, 2013

WOODS NDIO MWANAMICHEZO TAJIRI ZAIDI DUNIANI.

MCHEZAJI nyota wa mchezo wa gofu duniani, Tiger Woods ameendelea kuongoza orodha ya wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani kwa kukusanya kiasi cha paundi milioni 39.4 kwa mwaka. Woods ambaye akipambana kurejea katika kiwango chake toka atalikiane na mkewe mwaka 2010 mapato yake mengi yanatokana na mikataba minono aliyonayo katika makampuni mbalimbali ambayo amekuwa akitangaza bidhaa zao. Wengine katika orodha hiyo ni bondia kutoka Philipens, Manny Pacquiao anayekusanya kitita cha paundi milioni 37.7 kwa mwaka akifuatiwa na mchezaji nyota wa mpira wa kikapu katika ligi ya NBA ya Marekani Kobe Bryant anayekusanya paundi milioni 36.8 kwa mwaka. Nyota mwingine wa NBA LeBron James yuko katika nafasi ya nne akikusanya kiasi cha paundi milioni 36 akifuatiwa na nyota wa tenisi Roger Federer ambaye anakunja kitita cha paundi milioni 34.2 kwa mwaka wakati mcheza gofu mwingine Phil Mickelson yuko katika nafasi ya sita akipokea kitita cha paundi milioni 31.7 kwa mwaka. Nahodha wa zamani wa Uingereza ambaye kwasasa anacheza katika klabu ya Paris Saint-Germain yuko katika nafasi ya saba akikunja kitita cha paundi milioni 30.8 kwa mwaka na anafuatiwa na mchezaji bora wa dunia mara nne Lionel Messi ambaye yuko katika nafasi ya nane kwa kupokea kiasi cha paundi milioni 30. Dereva nyota wa mbio za magari ya langalanga Lewis Hamilton anashika nafasi ya tisa akijikusanyia kitita cha paundi milioni 30 na kumi bora inafungwa na bondia nyota wa uzito wa juu Floyd Mayweather anayekunja kitita cha paundi milioni 29.1 kwa mwaka.

No comments:

Post a Comment